Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (katikati) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakisaini Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, wakishuhudiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Onesphoro Gwajima (Mb), katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakibadilishana Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Nathan Belete, wakionesha Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) akizungumza baada yaTanzania na Benki ya Dunia, kusaini Hati ya Mikataba Miwili (2) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani sh. bilioni 248) kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania, maarufu kama “PAMOJA”, katika hafla iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
…………………..
Dar es Salaam, Desemba 12, 2024 – Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeweka msukumo mpya katika juhudi za kukuza usawa wa kijinsia baada ya kusaini mikataba yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104 (sawa na takribani shilingi bilioni 248). Fedha hizo zitaelekezwa kwenye utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia, maarufu kama PAMOJA, unaolenga kuboresha maisha ya wanawake Tanzania Bara na Zanzibar.
Mikataba hiyo imegawanywa katika msaada wa dola milioni 4 (sawa na shilingi bilioni 9.5) na mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 238)
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alieleza kuwa PAMOJA inalenga kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi kupitia vikundi vya biashara, huduma za kifedha rasmi, na fursa za masoko. Pia mradi huu utasaidia kuimarisha huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa kuwahudumia wanawake na wasichana.
“Mradi huu utawanufaisha wanawake 319,850 moja kwa moja na walengwa wengine 399,000 kutoka katika kaya za wanufaika. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa msingi wa taifa lenye haki na maendeleo,” alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuondoa vikwazo vinavyozuia maendeleo ya wanawake na kupanda mbegu za usawa kwa ajili ya kizazi kijacho.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema mradi wa PAMOJA unahusisha ujenzi wa nyumba 10 salama kwa watoto wanaokumbana na ukatili wa kijinsia na vituo 200 vya malezi bora, ambapo vituo 184 vitajengwa Tanzania Bara na 16 Zanzibar.
Dkt. Gwajima pia alibainisha kuwa fedha hizi zitatumika kuimarisha mazingira ya kazi ya maafisa maendeleo na ustawi wa jamii kwa kujenga ofisi 80 na kununua vifaa vya kazi, ikiwemo usafiri.
“Mradi huu unashughulikia changamoto ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya wanawake na familia zao. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuwainua wanawake kiuchumi,” alisema Dkt. Gwajima.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete, alisema kuwa wanatarajia mradi huu utaanza kutekelezwa haraka na kuleta matokeo yanayoonekana kwa walengwa. Alisisitiza kuwa mradi wa PAMOJA utasaidia kuondoa mila potofu, kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake, na kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Dkt. Nchemba alihimiza ukamilishaji wa masharti ya awali ili kuepusha ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi, ambao unaweza kusababisha gharama zisizohitajika.
Mradi wa PAMOJA unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo na kuimarisha usawa wa kijinsia nchini Tanzania, huku ukilenga kuweka msingi imara wa jamii yenye haki na ufanisi wa kiuchumi.