Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar no. 4 ya mwaka 2018 na Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Jamii ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 2015 ni miongoni mwa nyaraka muhimu za kisheria zinazotumika na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika kutekeleza majukumu yake ya msingi hasa ya uendeshaji wa Uchaguzi.
Kifungu cha 35 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kimetoa fursa kwa mwanamke kushiriki kupiga kura kwa vile kimebainisha watu wenye haki ya kupiga kura ambao ni kwa kila mtu alieandikishwa kuwa mpiga kura.
Hii ina maana raia wote wa kike na wakiume wenye sifa za kuandikishwa kupiga kura wanayo haki ya kupiga kura. Kinyume na Uchaguzi wa awali wa Zanzibar wa mwaka 1957 ni wanaume pekee ndio waliruhusiwa kupiga kura.
Vile vile sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar imetoa fursa kwa mwanamke kushiriki kugombea uongozi kwa nafasi za kisiasa, Wanawake wanayo fursa ya kugombea Urais, Uwawakilishi na Udiwani.
Asya Ali Seif mwanachama wa ACT Wazalendo anasema licha ya sheria hizo bado wanakabiliwa na vitisho wakati wa Uchaguzi“hii inatuonesha wazi kwamba tunafanyiwa danganya toto na wala haki zetu hazilindwi tunanyanyasika tu,
Hivi sasa wanawake wanajitoa tofauti na zamani katika kugombea lakini ukikumbuka vitisho vilivyopo na huku una familia hapo ndo wanawake wengine wanashindwa kugombea” ameeleza Asya.
Mwanasiasa wa NCCR Mageuzi Izack Mashaka anaamini kuwa sheria zilizopo zinahitaji kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa, “Serikali inapaswa kuimarisha sera za kijinsia ndani ya mfumo wa uchaguzi kwa kuhakikisha zinalenga moja kwa moja kuwawezesha wanawake kupata nafasi za kugombea kwa haki sawa,”
Aidha, anapendekeza ushirikishwaji wa wanawake katika utekelezaji wa sera, “Wanawake wanapaswa kushirikishwa zaidi kwenye uundaji wa sheria za uchaguzi ili kuzingatia changamoto wanazokabiliana nazo moja kwa moja nahimiza vyama vidogo kuonyesha mfano kwa kuwa na uwiano mzuri wa kijinsia kwenye orodha za wagombea wake”anasema Mashaka
Kifungu cha 35 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinaongeza ushiriki wa wanawake katika Baraza la wawakilishi na Mamlaka za serikali ya mitaa hadi ifikie 40% ya wajumbe wa kuchaguliwa.
Katika mikakati ya kusaidia kuongeza ushiriki na wanawake kwenye mzunguko wote wa uchaguzi ni uwepo wa Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Jamii ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliyoundwa baada ya kupata maoni ya wadau wa uchaguzi kuhusu ushirikishwaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika harakati za uchaguzi wa Zanzibar.
Kabla ya kuundwa kwa sera hii ushiriki wa makundi haya katika harakati za uchaguzi wa Zanzibar ulionekana ni mdogo sana, sera ya jinsia imekuja Kuweka mifumo itakayohakikisha usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa kijamii katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, pamoja na kuweka mikakati ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchaguliwa katika uongozi.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZNZ ni taasisi inayotetea haki za makundi mbalimbali ikiwemo wanawake, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dk Mzuri Issa anasema hofu ya usalama ni jambo linalozuia wanawake wengi kushiriki siasa “Wanawake hukumbwa na vitisho vya moja kwa moja vinavyohatarisha maisha yao na ya familia zao hili huwatisha hata wale walio tayari kugombea.”
Anasema kutokana na wanawake na makundi maalumu kuwa na wasi wasi na vurugu za uchaguzi “tunapendekeza kifungu kipya kinachozungumzia ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi ambacho kinaitaka tume kuwa na polisi mahususi kwa ajili ya uchaguzi na kuwapangia majukumu kwa namna ambavyo itafaa”anasema Mzuri
Mshauri elekezi na mchambuzi masuala ya utawala bora na mtetezi wa Demokrasia Ndg. Almas Suleiman anasema ili nchi iwe na demokrasia lazima isimamie yale ambayo wananchi wake wanayataka kwa mustakbali uliomzuri “ pia nchi iendeshe siasa safi kwa kila mmoja kusimama na kuwajibika kwa nafasi yake yakiwezekana haya demokrasia ya kweli itachukua nafasi yake na sio kuilazimisha kwa mabavu”anasema Almas
Afisa mipango na jinsia Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Lutfia Faida Haji anasema katika utekelezaji wa sera na sheria za uchaguzi ukosefu wa kifungu maalum cha sheria za kulinda wanawake dhidi ya ukatili wa uchaguzi ni changamoto kubwa “Sheria zilizopo hazijatoa ulinzi wa moja kwa moja kwa wanawake wanaoshiriki uchaguzi dhidi ya vitisho na kupelekea wanawake wengi kuhofia kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi”anasema Lutfia
Ameendelea kusema kuwa Vyama vya siasa vina jukumu kubwa katika kuhakikisha usawa wa kijinsia, “lakini vimekuwa vikiteua idadi ndogo ya wagombea wanawake, na mara chache mwanamke hupendekezwa kugombea hali hii inadhoofisha jitihada za kuwajumuisha wanawake kwenye uongozi wa juu wa nchi.”anamalizia Lutfia
Bimkubwa Bereki mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMAanasema katika utekelezaji wa sera na sheria za uchaguzi, ni lazima tuhakikishe kuwa vyama vinaweka mazingira rafiki kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi “ Pia vyama vina jukumu la kuimarisha usaidizi wa kifedha kwa wagombea wanawake kupitia rasilimali za chama bila hivyo sera hizi zitabaki kwenye karatasi bila matokeo halisi,”
Aidha ametaja haja ya mabadiliko ya kisheria ili kulinda wanawake dhidi ya ukatili wa kisiasa kwa kusema “Hakuna maana ya kuwa na sheria za uchaguzi kama haziwalindi wanawake dhidi ya vitisho na manyanyaso tunahitaji vifungu maalum vya sheria vitakavyowalinda wanawake wanaoshiriki uchaguzi,” ameeleza Bereki.