Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inaendelea na tathmni ya uwepo wa magugu maji katika Ziwa Victoria ili kupatia ufumbuzi changamoto hiyo.
Mhe. Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Januari 31, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini Mhe. Constantine John Kanyasu aliyetaka kujua kama Serikali inafahamu ongezeko la magugu maji katika Ziwa Victoria, zipi ni athari za magugu hayo na mpango wa kuyadhibiti.
Amesema Serikali imechukua jitihada za kudhibiti magugu maji katika ziwa hilo ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa na kutekeleza Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka 2019-2029 ambao unatoa mwongozo wa namna ya kuzuia kuingia na kuenea kwa viumbe vamizi na una mipango endelevu ya kushughulikia viumbe vamizi waliopo na wale wanaoweza kuingia.
“Mheshimiwa Spika, tathmnini inaendelea na nimuombe Mheshimiwa Bunge avute subira wakati tunaendelea kulishughulikia jambo hili kwani limeendelea kuathiri vyanzo vingi vya maji nchini kwa mfano Ziwa Jipe nalo lina changamoto ya kuzingirwa na maji,” amesema Mhe. Khamis.
Ameongeza kuwa Serikali inawajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na ziwa kuhusu namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza na kuenea kwa magugu maji kila yanapojitokeza ikiwemo kung’oa, kukausha na kuchoma magugu maji na kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kudhibiti uharibifu mifumo ikolojia ya Ziwa Victoria.
Aidha, magugu maji yanaleta athari kwa mazingira, uchumi na kijamii ikiwemo kupungua kwa oksijeni kwenye maji ambayo huzuia mzunguko wa hewa na mwanga wa jua na hii husababisha vifo vya samaki na viumbe wengine wa majini, uharibifu wa mifumo ikolojia na bioanuai ya Ziwa Victoria na huathiri maeneo ya mazalia ya Samaki, shughuli za uvuvi na usafirishaji.