Na John Mapepele
Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa operesheni maalum ya doria inayoendelea Wilayani Itilima kudhibiti fisi katika maeneo hayo inayoshirikisha Askari wa Uhifadhi na wananchi wa maeneo hayo kwa siku kadhaa sasa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora doria ya kudhibiti fisi inaendelea katika eneo la milima ya Kagera, Kijiji cha Itilima, Kata ya Nyamalapa, Wilaya ya Itilima lengo ni kudhibiti fisi hao wanaodaiwa kuwasumbua wananchi katika maeneo yote ya wilaya hiyo.
“Lengo la doria hii ni kufanya ukaguzi kwenye eneo la milima hiyo ambapo inadaiwa na wananchi wa eneo hilo kuwa ni maficho ya fisi” amesisitiza Dkt. Labora.
Aidha, amefafanua kuwa doria maalum kama hizo ni endelevu kwa maeneo yote nchini ambapo yataonekana kuwa na wanyama hatarishi kwa jamiii ili kuwalinda wananchi wasiweze kusumbuliwa.
Amesema katika doria hiyo, mwenyekiti wa kijiji cha Lali Kata ya Lagangabilili wilaya ya Itilima Kija Genge amewaongoza wananchi wake kushirikiana kwenye doria na kikosi maalum cha Askari wa Uhifadhi wa Maliasili na Utalii katika eneo la milima ya Lali.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hassan Abbasi amefafanua kwamba Wizara itaendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na wanyama wakali na wahalibifu katika maeneo yote nchini na ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanaposumbuliwa ili waweze kupata msaada wa haraka wakati wowote.
” Wizara imejipanga kikamilifu kukabiliana na wanyama wakali na wahalibifu wakati wowote, hii kwetu kama Serikali ni ajenda ya kudumu”. Amefafanua, Dkt. Abbasi