Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Pili la Utalii wa Vyakula barani Afrika, linaloratibiwa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), Aprili 25, 2025, jijini Arusha. Tukio hili litakutanisha zaidi ya wadau 300, wakiwemo viongozi wa sekta ya utalii, wataalam wa vyakula, na wawakilishi wa serikali kutoka mataifa mbalimbali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amesema uamuzi wa kuipa Tanzania uenyeji ulifikiwa kutokana na urithi wake wa kipekee wa vyakula vya asili na utamaduni wa upishi. “Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyeji baada ya jukwaa la kwanza lililofanyika Victoria Falls, Zimbabwe, Julai 2024,” alisema.
Jukwaa hilo litaangazia nafasi ya utalii wa vyakula katika kukuza uchumi na kuhifadhi utamaduni. Pamoja na mijadala ya jopo, kutakuwa na maonesho ya mapishi, vipaji vya wapishi wa ndani na nje, pamoja na maonyesho ya vyakula vya Kiafrika.
Mkurugenzi wa UN Tourism Kanda ya Afrika, Elcia Grandcourt, amesema kuwa jukwaa hilo litatoa fursa kwa wageni kuonja na kufurahia ladha ya vyakula vya Kiafrika. “Nimeshajaribu nyama choma na ugali wa Kitanzania, na nina hakika tukio hili litaleta uzoefu wa kipekee kwa washiriki,” alisema Grandcourt.
Serikali ya Tanzania inashirikiana na UN Tourism na Basque Culinary Center kuhakikisha jukwaa hilo linafanikiwa, huku wadau wa utalii wakihimizwa kuchangamkia fursa zinazotokana na tukio hilo.