Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndg. Fue Mrindoko akipandisha bendera ya CCM wakati akizindua Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndg. Fue Mrindoko, amezindua Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha, pamoja na kupokea wanachama wapya 50 kutoka Jumuiya ya Wazazi, katika kata ya Kolandoto.
Mrindoko amezindua Shina hilo la Wajasiriamali leo, Jumamosi Februari 23, 2024, akiwa katika ziara yake akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Ziara hiyo imehusisha kutembelea kata za Chamaguha, Ibadakuli, na Kolandoto kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na uhai wa chama.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mrindoko amesema kuwa ufunguzi wa shina hilo utawezesha wajasiriamali hao kupata mikopo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, na hivyo kujiinua kiuchumi.
Kupokea Wanachama Wapya
Mrindoko amewapongeza wanachama wapya walioungana na Jumuiya ya Wazazi CCM katika kata ya Kolandoto na kusisitiza kuwa uhai wa CCM unategemea idadi kubwa ya wanachama, hasa wanaolipa ada za uanachama.
Ukaguzi wa Miradi ya Ujenzi
Akiwa katika kata ya Ibadakuli, Mrindoko, pamoja na wajumbe wa kamati ya utekelezaji, wametembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa matundu ya vyoo na mabweni katika Shule ya Sekondari Rajani.
Amewataka wakandarasi wa miradi hiyo wahakikishe wanakamilisha kazi zao kwa wakati, akisema tarehe ya mwisho ya Machi 10 ,2025 aliyoahidi kukamilisha kazi iwe ya kweli.
Wito wa Wazazi na Walezi
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji, Daniel Kapaya, amewahimiza wazazi na walezi kuchukua hatua madhubuti kulinda watoto wao na kuhakikisha wanapata lishe bora ili waweze kukua vizuri.
Amewataka wazazi kutoa chakula cha mchanganyiko kwa watoto shuleni ili kudhibiti utapiamlo.
“Akina mama naomba tunyonyeshe watoto wetu, lakini pia tuwape chakula wanafunzi shuleni. Wazazi mnakula zaidi ya watoto, naomba msiwe wachoyo, msiwapunje watoto chakula, changieni chakula shuleni lakini pia tuhakikishe tunawapa watoto chakula mchanganyiko ili kukabiliana na utapiamlo”,amesema Kapaya.
Afya ya Jamii
Mjumbe mwingine, Boniphace Giti, amehimiza wananchi kufanya mazoezi na kutumia huduma za hospitali na vituo vya afya ili kufanya uchunguzi wa afya zao mapema, badala ya kutegemea waganga wa kienyeji.
Maoni ya Wajumbe
Wajumbe wengine wa Kamati ya Utekelezaji, Zulfa Hassan, Mary Makamba, na Mhandisi James Jumbe, wamesisitiza kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Wamesisitiza kuwa “Wajibu wa Makada wa CCM ni kuyasema mazuri yote anayofanya Rais Samia.”
Usajili wa Wanachama
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi, amesisitiza umuhimu wa vikao vya kikatiba na kikanuni, pamoja na kuhamasisha usajili wa wanachama wapya ili kuendeleza idadi ya wanachama na kuongeza nguvu ya chama.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndg. Fue Mrindoko (wa pili kushoto), akizindua Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndg. Fue Mrindoko akipandisha bendera ya CCM wakati akizindua Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Kibabi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha










