Na Nihifadhi Abdulla
Katika jamii nyingi, ndoa imekuwa taasisi muhimu inayotambulika kwa kuimarisha familia na jamii kwa ujumla, katika muktadha wa usawa wa kijinsia, ndoa pia imekuwa kizuizi kwa wanawake wanaotamani kushiriki katika siasa na uongozi.
Ingawa kuna maendeleo katika kuhakikisha usawa wa kijinsia, bado kuna changamoto zinazoathiri wanawake walio ndani ya ndoa, hasa pale ambapo waume zao hawaungi mkono ndoto zao za kuwa viongozi.
Wanawake Walionyimwa Nafasi ya Uongozi kwa Sababu ya Ndoa
Joyce Banda, aliyekuwa Rais wa Malawi, alikumbana na vikwazo vingi kutoka kwa mume wake wa kwanza, ambaye alihisi kuwa mwanamke hastahili kushiriki katika siasa. Banda alilazimika kuachana na ndoa hiyo ili kufuata ndoto yake ya kuwa kiongozi. Hali yake inaakisi changamoto zinazowakumba wanawake wengi wanaotaka kushiriki katika siasa lakini wanakutana na vikwazo kutoka kwa waume zao.
Phumzile Mlambo-Ngcuka aliyewahi kuwa Naibu Rais wa Afrika Kusini, alikiri hadharani kuwa wanawake wengi walio katika ndoa hupata ugumu wa kushiriki katika siasa kwa sababu ya mitazamo ya waume zao. Hali hii ilimlazimu kupambana na dhana potofu kwamba uongozi ni jukumu la wanaume pekee.
Wanawake wengine wasiojulikana
Mbali na wanawake mashuhuri, kuna wanawake wengi wa kawaida ambao huteseka kimya kimya kwa sababu waume zao kupinga ushiriki wao katika siasa na uongozi.
Katika tafiti mbalimbali, zimebainisha kuwa wanaume wengi huathiri maamuzi ya wake zao kwa mtazamo kwamba mwanamke bora ni yule anayebaki nyumbani na kulea familia.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women), ulibaini kuwa asilimia 65 ya wanawake walio ndani ya ndoa hukumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa waume zao wanapojaribu kushiriki katika siasa.
Masha khalfan mkaazi wa kinuni anasema baada ya kupata mafunzo mbalimbali ya uongozi akawa na nia ya kugombea nafasi ya uongozi lakini imefutika badala ya mume wake kumuekea vikwazo na hivyo kuamua kujitoa na kuendelea kutunza familia.
”nilishajijengea imani kwenye chama na wengi walinikubali baada ya kumshrikisha baba watoto(mume) hajakubaliana nami na kunitaka nichague ndoa au uongozi, nikiangalia watoto nikaamua iwe basi tangu apo nikaacha kugombea ata nafasi kikundi”anamalizia Masha
Mikataba na tafiti zinazothibitisha hali hii
Mkataba wa CEDAW (Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women) huu ni mkataba wa kimataifa unaopinga ubaguzi dhidi ya wanawake. Licha ya kuwepo kwa mkataba huu, bado kuna changamoto katika utekelezaji wake, hasa ndani ya ndoa ambapo wanawake wanazuiwa kushiriki katika uongozi.
Utafiti wa UN Women (2022) umeonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake waliokatisha safari yao ya kisiasa walitaja ndoa kama chanzo kikuu cha changamoto zao.
Ripoti ya World Economic Forum (2023) inasema kuwa katika nchi nyingi za Afrika, wanawake walioolewa wana nafasi finyu ya kushika nyadhifa za uongozi ukilinganisha na wale wasio na ndoa.
Njia za Kusaidia Wanawake Kupata Nafasi ya Uongozi
Mkurugenzi idara ya maendeleo wanawake na watoto Zanzibar Siti Abass Ali anasema kinachohitaji ni utoaji wa elimu na uhamasishaji “wanawake wanapaswa kufahamu kuhusu haki zao ili waweze kujitetea dhidi ya vikwazo vya ndoa na bila ya utoaji wa elimu ya kina itakuwa ngumu kufikia lengo”anasema Siti.
Almas Suleiman mshauri elekezi masuala ya utawala bora na mtetezi wa Demokrasia anasema ni vyema kuwepo mabadiliko ya Sheria “taasisi husika zinapaswa kuweka sera zitazowalinda wanawake dhidi ya vikwazo vya kifamilia wakati wanapojihusisha kuwania nafazi za uongozi”
“kuna wanawake ambao wanania kugombea nafasi za uongozi lakini wanaogopa kuingia kwenye ndoa kwasababu wanaona ndoto zao zitafikia tamati” anasema Almas
Pamoja na hayo anaeleza kuwa ili kuondosha vizuizi hivyo wanaume wanapaswa kupewa mafunzo kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia ili wawe sehemu ya suluhisho na kuwaunga mkono badala ya kuwa kikwazo dhidi ya wanawake kwenye adhma ya uongozi.