Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dkt Khalid Salum Muhammed ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini ZMA kufanya kazi kwa ari na kujitoa ili kuweza kufikia malengo ya taasisi hiyo.
Ameyasema hayo wakati akizindua Bodi ya saba ya Wakurugenzi, katika ukumbi wa Ofisi ya Mamlaka hiyo Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi.
katika hutuba yake kwa bodi na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini dk khalid amesema ni vyema kufanya kazi kwa mashirikiano na kuitaka bodi hiyo kulisimamia hilo.
Aidha amesema kuwepo kwa bodi hiyo itakwenda kuwa daraja kati ya Wizara ya mawasiliano na uongozi wa Mamlaka hiyo, hivyo nilazima kufanya kazi kwa uwajibikaji na kwa uaminifu ili kuweza kuendeleza taasisi hiyo.
“Bodi hii ni kiungo kati ya wizara na uongozi wa ZMA hivyo nilazima tufanye kazi kwa mpangilio uliopo kwa uwajibikaji,uaminifu na bila muhali tunaweza kuendeleza taasisi hii”
Hatahivyo ameeleza kuwa taasisi hiyo ni kubwa na inakazi kubwa ya usimamizi wa vyombo vya bahari ikiwemo Meli,Maboti na Vyombo vidogovidogo vya baharini hivyo ni vyema kuendeleza kazi hizo kwa ufanisi.
Hatahivyo amesema zaidi ya asilimia 90 ya sehemu ya uchumi wa buluu inafanyiwa kazi katika taasisi hiyo hivyo ni vyema Uongozi wa bodi hiyo na wafanyakazi wa mamlaka hiyo, wafanye kazi kwa ufanisi ili waweze kufanya haki ya usimamizi wa mamlaka hiyo.
Vilevile Dkt Khalid amewakumbusha wafanya kazi wa ZMA kuwa waadilifu na kujiepusha na jambo lolote litakalochochea rushwa kwenye Mamlaka hiyo.
kulikua na madeni hayasimamiwi ipasavyo hivyo ni wajibu kwa wanyakazi hao kuweza kuibadilisha ZMA kwani nilazima kufanya kazi kwa kujitolea na kwa uzalendo.
Aidha amewataka wafanya kazi hao kuacha kufanya kazi kwa Fitna na majungu kwani ndio chachu ya kudumaza maendeleo katika kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Ndugu Mtumwa Said Sandal ameiomba bodi ya wakurugenzi kumpatia mashirikiano ili kusimamia vizuri majukumu ya taasisi hiyo.
Nae Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ndg Mustafa Aboud Jumbe amesema watazifanyia kazi nasaha za waziri huyo kwani wanakazi kubwa ya kutekeleza majumu ya taasisi hiyo kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Mamlaka ya usafiri baharini imezindua bodi yake ya saba ya wakurugenzi ambapo msisitizo mkubwa umewekwa kwenye mageuzi ya kidigital katika mifumo ya usajili wa vyombo vya baharini ili kuengeza ufanisi na uwazi katika kazi za Mamlaka hiyo.