Na Prisca Libaga, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Jumatatu Machi 03, 2025 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, ametimiza ahadi yake, kwa kumkabidhi Bibi Arafa Yusuph Matoke Bajaji mpya pamoja na Runinga chapa ya Toshiba smartTv inchi 43.
Jana Jumapili wakati wa michezo mbalimbali kwa wanawake, ikiwa ni shamrashamra za kuelekea kwenye Kilele cha Siku ya wanawake duniani, ambayo Kitaifa yatafanyika Jijini Arusha,Mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Bi. Arafa Mwenye miaka 74, alimkosha Mhe. Makonda kiasi cha kuomba amsikilize zawadi anayoitaka kama sehemu ya motisha kwa wanawake wengine kuweza kujitokeza kwenye shughuli mbalimbali za Kijamii.
Mhe Mkuu wa Mkoa katika maelezo yake wakati wa kukabidhi Bajaji hiyo, amesema yote anayoyafanya Mkoani hapa anayepaswa kushukuriwa ni Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake, imani na uteuzi alioufanya kwa Mhe. Makonda, kuona kuwa anaweza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Bajaji iliyokabidhiwa leo kulingana na Mhe. Makonda imetolewa na Benki ya NMB.


