Mratibu wa RITA mkoa wa Arusha Philemon Mkwai wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililoko kwenye viwanja vya TBA mkoani Arusha
………..
Happy Lazaro, Arusha .
Wananchi wametakiwa kutumia huduma ya e RITA kwani inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati na kwa haraka mahali popote na kwa muda wowote na kuweza kusaidia serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kuboresha huduma zingine za kijamii.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mratibu wa RITA mkoa wa Arusha Philemon Mkwai wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililoko kwenye viwanja vya TBA mkoani Arusha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma hiyo kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani machi 8 mwaka huu.
Amesema kuwa ,eRITA ni mfumo unaokuwezesha kutuma maombi ya huduma ya vizazi,vifo,ndoa,talaka na udhamini kwa njia ya kidijitali popote ulipo.
Amefafanua kuwa, eRITA ni rahisi kutumia salama na itakuwezesha kupata huduma kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Aidha ametaja huduma zinazopatikana eRITA kuwa huduma za vizazi,vifo,ndoa na talaka, na udhamini.
” huduma hizi zote zinatolewa kwa njia ya kidijitali na inafanywa na mwananchi mwenyewe popote pale alipo na uwepo wa huduma hii imeturahisishia kuondoa msongamano wa foleni ya watu kwenye ofisi zetu kwani kila kiti kinafanyika kidijitali. “amesema.
Amesema kuwa, uwepo wa huduma hiyo umesaidia pia kutoa huduma nyingi zaidi na kwa wakati ambapo mtoa huduma kwa sasa hivi anahudumia watu mia moja hadi mia tatu kupitia huduma hiyo kwa sasa tofauti na hapo awali .
“Matumizi ya huduma hii tumeshatoa elimu maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijijini na bado tunaendelea kutoa elimu zaidi kwani kwa wale ambao hawana simu zenye uwezo huo hasa maeneo ya vijini wanaweza kupata huduma hiyo kwa haraka kwenye vituo vya afya kwa wakati huo huo .”amesema.