Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman, amezitaka taasisi zenye uwezo kutafuta miradi ya kuwawezesha makundi maalum ili yawajibike kiuchumi na kuepukana na utegemezi.
Waziri Suleiman alitoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi futari kwa familia 800 za watu wenye ulemavu, hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Nour Al-Yaqin Foundation katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohammed Shein, Tunguu, Zanzibar.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa watu wenye ulemavu, wajane, mayatima na wasiojiweza mara nyingi hupewa misaada ya mahitaji ya msingi ambayo hutumika na kuisha, hivyo kubaki wakisubiri msaada mwingine.
“Umefika wakati wa taasisi kuangalia miradi mbadala inayoweza kuwasaidia kujiendesha kimaisha na kukidhi mahitaji ya familia zao. Wapo wenye ulemavu wanaoweza kufanya kazi na kujipatia kipato endapo watawezeshwa,” alisema Waziri Suleiman.
Aliongeza kuwa jitihada hizo zitasaidia kukuza uchumi wa makundi hayo, kupunguza utegemezi, na hata kuwafanya wawe sehemu ya kusaidia wengine. Pia alibainisha kuwa serikali inaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha jamii ya watu wenye ulemavu inabaki salama na yenye fursa sawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika kusaidia serikali kufikisha huduma kwa makundi maalum. Aliipongeza Nour Al-Yaqin Foundation kwa kushirikiana na serikali katika kuwasaidia wananchi wasiojiweza, ikiwemo watoto yatima na watu wenye ulemavu, na kuzitaka taasisi nyingine kuunga mkono juhudi hizo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu, Mhandisi Ussi Khamis Debe, aliishukuru taasisi hiyo kwa misaada yao Zanzibar, akieleza kuwa kwa miaka minne wamekuwa wakipokea sadaka kutoka kwao. Kwa mwaka 2025, watu 1,000 wenye ulemavu wamepangwa kunufaika na misaada hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Nour Al-Yaqin Foundation, Makame Salim Ali, alisema kwa mwaka 2025 taasisi hiyo imesaidia watu 2,000 wenye hali ngumu katika mikoa tofauti ya Zanzibar, wakiwemo watu 1,000 wenye ulemavu.
Akizungumza kwa niaba ya wafadhili wa sadaka hizo, Hakal Vurel, Mjumbe wa Bodi ya International Humanitarian Relief Organization (IHHNL), alisema taasisi yao inatoa misaada katika nchi 39 na itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar ili kuboresha maisha ya jamii.
Baadhi ya wananchi waliopokea msaada huo, wakiwemo Naima Hemed Hamad, Fatma Zahor, Suleiman Makame na Mwanajuma Yazid Yussuf, waliomba taasisi nyingine kuendelea kusaidia Waislamu wasio na uwezo hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, wakiamini kuwa malipo makubwa ni kutoka kwa Allah.
Misaada hiyo imetolewa kwa ufadhili wa International Humanitarian Relief Organization (IHHNL), Stichting Bir Dua na Stichting IBA kutoka Uholanzi kupitia Nour Al-Yaqin Foundation iliyopo Zanzibar.