WATUMIAJI wa pikipiki hususani bodaboda wametakiwa kufuata sheria za barabarani na
kuzingatia matumizi sahihi ya pikipiki kama wanavyoshauri wataalamu ili
zidumu kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Albert Chalamila, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, wakati akizindua pikipiki za kampuni ya Alternative Solution Limited, ambao ndio wasambazaji wa pikipiki za Daima na Everlast.
“Inapendeza kabisa kuona sisi watanzania wenyewe tukitafuta suluhisho ili kuleta unafuu katika sekta hii ya usafirishaji kwani pikipiki zinatumika kila mahali nchini na zinarahisisha usafiri wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine,” alisema.
Alitoa wito kwa watumiaji wa pikipiki hususani bodaboda kufuata sheria za barabarani na kuzingatia matumizi sahihi ya pikipiki kama wanavyoshauri wataalamu ili zidumu kwa muda mrefu. “Tunao wataalamu hapa leo naomba tuwasikilize ili matumizi yawe bora na pamoja na mambo mengine tupunguze ajali,” alisema.
Alitoa wito kwa mashirika mbalimbali ya kifedha yaingie makubaliano na Alternative Solution Limited ili kuhakikisha waendesha boba boda wengi wanajengewa uwezo wa kumiliki pikipiki zao wenyewe kwa utaratibu mzuri usiowaumiza.
Kwa mujibu wa Mh. Chalamila tayari Jiji la Dar es Salaam limeanza kufanya kazi saa 24 na moja ya usafiri unaotegemewa na watu wengi ni pikipiki. “Uzinduzi huu umekuja muda mwafaka wakati bidhaa hii inahitajika,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Alternative Solution Limited, Bw. Ruge Chacha alisema kampuni hiyo ilifanya utafiti wa kina ili kujua mahitaji ya watanzania hususani watumia pikipiki na changamoto wanazopitia kabla ya kuziagiza.
Alisema pikipiki za Daima na Everlast zina faida nyingi zaidi ikilinganishwa na pikipiki nyingine ikiwemo kuwa na nafasi kubwa ya kukalia kwa dereva pamoja na abiria lakini pia pa kubebea mizigo, sehemu ya kuhifadhi na kuchajia simu, sehemu ya kuwekea chupa ya maji upande wa kulia na taa imara inayoona vizuri hata wakati wa mvua na giza.
Bw Chacha alibainisha kuwa piki piki hizo zina zina matairi imara kabisa yanayowezesha kupakia abiria na mzigo mzito bila wasiwasi yoyote kwani kuna sehemu maalumu ya mizigo ambayo pikipiki nyingine hazina kabisa.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau zaidi ya 300 wa sekta ya usafirishaji hususan pikipiki na baadhi walipata fursa ya kujaribisha na kuuliza maswali kuhusu pikipiki hizo mpya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mh. Dorothy Kilave aliahidi kuendelea kushirikiana na waendesha boda boda wote Kwa kuzingatia umuhimu wao katika jamii.
“Zingatieni Sheria za barabarani na mnunue pikipiki za Daima na Everlast zitawasaidia,” alisema.
Baada ya uzinduzi huo piki piki hizo za Daima na Everlast zitasambazwa nchi nzima kupitia mawakala tofauti tofauti.