Na John Bukuku, Bunju Dar es Salaam.
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuwa na taasisi inayosimamia na kuratibu biashara ya kaboni kisheria, hatua inayotarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa nchi. Hatua hii itatoa fursa kwa Tanzania kushiriki katika masoko ya kaboni kimataifa, kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali, na kuongeza pato la Taifa.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Yusuf Masauni ili kufungua mkutano huo ameelezea namna umuhimu wa kuwa na taasisi hiyo kwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
Amesema zaidi ya hayo, usimamizi thabiti wa biashara ya kaboni utasaidia kulinda mazingira dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa gesijoto. Pia, utachochea ushirikiano kati ya serikali, taasisi binafsi, na mashirika ya kimataifa katika kuibua fursa mpya za uwekezaji kwenye sekta hii.
Mhandisi Masauni amefafanua kuwa Takwimu zinaonyesha kuwa kufikia Februari 2025, jumla ya maombi 71 ya miradi ya biashara ya kaboni yamepokelewa. Miradi hiyo inahusisha utunzaji wa misitu ya asili na ya kupanda, nyanda za malisho, kilimo mseto, nishati, na udhibiti wa taka ngumu. Miradi hii inatarajiwa kuchangia pato la Taifa kwa wastani wa Dola bilioni 1 za Marekani (sawa na shilingi trilioni 2.4) kwa mwaka kupitia mauzo ya viwango vya kaboni.
Alieleza kuwa mkutano huo unalenga kujenga uwezo wa taasisi za umma na mashirika kushiriki ipasavyo kwenye fursa zinazotokana na biashara ya kaboni. Pia, mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera na mikakati madhubuti ya kuboresha usimamizi wa sekta hiyo.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujifunza kuhusu mabadiliko ya tabianchi, mbinu za kupunguza uzalishaji wa gesijoto, na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika uwekezaji wa biashara ya kaboni. Serikali imesisitiza dhamira yake ya kusaidia utekelezaji wa sera na mikakati madhubuti ili kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira na kukuza uchumi wa Taifa.