Na FARIDA MANGUBE MOROGORO
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Omari Selemani Mwanamtwa, dereva teksi, kwa tuhuma za kumuua mwanamke aliyefahamika kwa jina la Ulumbi Stephano, mkazi wa Kihonda, tukio lililotokea mwaka 2016.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema mtuhumiwa anadaiwa kutekeleza mauaji hayo mnamo Machi 2016 katika eneo la Kasanga Mashambani, Manispaa ya Morogoro.
“Tukio la kifo cha mwanamke huyo lilivuta hisia za watu wengi wakati huo, kwani ilidaiwa kuwa aliuwawa na mwili wake haukuweza kuonekana mpaka sasa,” amesema Kamanda Mkama.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa marehemu alikuwa na mazoea ya kutumia gari la mtuhumiwa kwa shughuli zake binafsi za matembezi kutokana na hali yake ya ulemavu wa miguu.
Kamanda Mkama ameendelea kueleza kuwa baada ya mwanamke huyo kutoonekana kwa muda, gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T.577 AQJ, ambalo lilikuwa likiendeshwa na mtuhumiwa na kumilikiwa na Mayasa Alli Hashimu, aliyekuwa Afisa Elimu na mkazi wa Tanga, lilikutwa limetelekezwa eneo la Msamvu, katika kituo cha kuuzia mafuta.
Aidha, amesema kuwa katika kipindi chote hicho, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi limekuwa likifuatilia kwa kina tukio hilo hadi hatimaye mtuhumiwa amekamatwa. Hata hivyo, mwili wa marehemu bado haujapatikana.
_”Tunaendelea kukamilisha taratibu za kisheria kwa ajili ya hatua zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa gari la mtuhumiwa lilikutwa na damu iliyodhaniwa kuwa ya marehemu Ulumbi Stephano” amesema kamanda Mkama.