Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni akizungumza na vyombo vya habari kuhusu zoezi la Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu nchini Tanzania wakati wa Mkutano wa 11 wa Petroli wa Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni akifanya wasilisho kwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya petroli kuhusu vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia zinavyonadiwa, wakati wa Mkutano wa 11 wa Petroli ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaoendelea jijini Dar es Salaam.
………………..
Dar es Salaam
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imejipanga kuweka msukumo mkubwa kwenye utafutaji wa gesi asilia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha uwekezaji na matumizi ya nishati jadidifu.
Akizungumza katika Kongamano la 11 la Mafuta na Gesi la Afrika Mashariki (EAPCE25) linaloendelea jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, alisema kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali inalenga kuongeza juhudi katika utafutaji wa gesi ili kuendana na mabadiliko ya nishati duniani.
“Malengo ya dunia ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2050, sekta ya nishati imebadilika kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana Wizara ya Nishati imeendelea na mazungumzo na wadau waliogundua gesi baharini, ili kuhakikisha kuwa gesi hiyo inatengenezwa kuwa LNG kwa ajili ya kuuza kwenye masoko ya kimataifa, ikiwemo Japan, Korea, na Taiwan,” alisema Sangweni.
Aliongeza kuwa Tanzania tayari imegundua akiba ya gesi asilia yenye futi za ujazo trilioni 57.54, na jitihada zinaendelea ili kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye vitalu vilivyotengwa kwa ajili ya utafutaji wa gesi. Kwa mujibu wa PURA, nchi ina vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi, ambapo 23 vipo baharini na vitatu vipo katika eneo la Ziwa Tanganyika.
Sangweni aliwahimiza wawekezaji kutembelea banda la PURA katika maonyesho hayo ili kupata taarifa za kina kuhusu fursa zilizopo, huku akibainisha kuwa serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuharakisha maendeleo katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki pamoja na wakuu wa taasisi za serikali na makampuni yanayohusika na sekta ya mafuta na gesi.