Na Belinda Joseph, Ruvuma.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma limetowa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme ili kudhibiti wizi wa nyaya za kopa kwenye transfoma, ambao huleta changamoto katika ya ukosefu wa huduma ya umeme kwani ni moja ya uharibifu mkubwa.
Katika mwendelezo wa ziara ya Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro, ametembelea kijiji cha Mkurumusi Kata ya Mpitimbi, Wilaya ya Songea, ambapo amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hiyo kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na wizi wa nyaya za umeme, huku akisisitiza kuwa wizi wa nyaya hautaathiri TANESCO pekee, bali pia jamii kwa ujumla itapata madhara ya ukosefu wa huduma ya umeme.
Njiro amewataka wananchi kutoa taarifa za haraka pindi watakaposhuhudia watu wasiofanya kazi na Shirika hilo wakiwa kwenye transfoma, wasiwafiche wahalifu kwani jamii kwa ujumla itakosa huduma ya umeme, jambo linaloweza kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Msaidizi Bi. Emma Ulendo, amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishwa na umeme pindi huduma hiyo itakapozinduliwa rasmi kijijini hapo, huku akisisitiza kuwa malipo ya huduma hiyo yafanyike kwa njia rasmi kupitia namba ya kumbukumbu ya malipo (Control Number) ili kuepuka udanganyifu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpitimbi, Kassian Kayombo, alieleza kuwa wanatarajia kupata manufaa makubwa kutoka huduma ya umeme, na aliishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa umeme katika kuboresha maisha ya wananchi.