Baadhi ya wanawake kutoka katika taasisi mbalimbali walioshiriki katika maandamano ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa:Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile amewataka wanawake kuacha uoga na kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kuwa wanaweza.
Nyakia amesema hayo leo March 8,2025 wakati akizungumza na wanawake wa Manispaa ya Sumbawanga katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela.
Nyakia amesema wanawake Wana nafasi kubwa ya kushiriki kwenye uchaguzi kwa kuwa wanauwezo ujasiri na nguvu katika kutenda jambo lolote.
Amewataka wanawake kuendelea kukemea vikali vitendo vya ukatili kwa watoto na kupinga rushwa ya ngono.
Aidha amewasisitiza wanawake kujitokeza kwenye nafasi mbalimbali za uchaguzi maana wao ndio wanaokutana na changamoto nyingi katika Jamii hivyo ushiriki wao utasaidia kutatua matatizo yanayojitokeza kwenye Jamii.
Awali akizungumza na wanawake Mbunge wa jimbo la Sumbawanga Aesh Halfan Hilary amesema kuwa ushiriki wa wanawake katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ni nafasi kwa wanawake kuweza kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Pia Aesh amewataka wanawake kuunda vikundi vitakavyowasaidia kupata mikopo na kujiinua kiuchumi.
Nao baadhi ya wanawake akiwemo Agatha Maliyawatu amesema siku ya wanawake inaibua fursa mbalimbali ambazo zinawakutanisha pamoja.
“Tunaiomba Serikali kutumia siku hii kwa kuwafanya watoto wa kike walioko shule kujitambua na kutambuliwa thamani yao.”amesema Maliyawatu.
Siku ya wanawake duniani huadhimishwa tarehe 8 ,mwezi wa tatu kila mwaka ,ambapo kwa mwaka huu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kitaifa yamefanyika jijini Arusha na mgeni rasmi ni Rais wa jamhuri ya muungano wa Rukwa Dkt Samia Suluhu Hassan.