Na Sabiha Khamis Maelezo
Vijana wametakiwa kutambua na kujua historia ya nchi kwa kuyaenzi na kuyalinda mazuri yaliyoachwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ili kuendelea kuiweka nchi katika hali ya amani na utulivu.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Mhe. Shamata Shaame Khamis katika ziara ya kusoma dua ya aliekuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Chama cha Afro – Shirazi Marehemu Sheikh Thabit Kombo Chukwani wilaya ya Magharib B, amesema Marehemu Sheikh Thabit alikuwa na mchango mkubwa katika kuijenga nchi kwa kushika nyadhifa mbali mbali Serikalini.
Amesema hatua iliyofikiwa hivi sasa katika nchi ni miongoni mwa matunda yaliyoachwa na viongozi ambao wamepigania uhuru wa nchi kwa ajili ya kuikomboa Zanzibar na kuwaweka huru Wazanzibar ili kujiletea maendeleo.
Aidha Mhe Shamata amefahamisha kuwa, Serikali kwa kuthamini mchango wa viongozi hao imeona ni jambo jema kwa kuweka utaratibu wa kuwatebelea na kusoma dua katika makaburi ili kuendelea kuwaenzi Viongozi hao.
Hata hivyo amesistiza kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliopo ili kuendelea kudumisha amani na utulivu ambayo imetafutwa na waasisi wa nchi kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mjukuu wa Marehemu Sheikh Thabit Kombo Ndugu Muhideen Muhsin Ali amesema wanafamilia wamefarijika kwa kuona viongozi waasisi hao wanathaminiwa pamoja na kuenziwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa utaratibu wa kuwatembelea na kuwaombea dua kila mwaka.
Hata hivyo ameiomba Serikali kuliendeleza jambo hilo kila mwaka ili kusaidia vizazi vijavyo kujua historia ya waasisi na viongozi waliopigania uhuru wa nchi.
Ni muendelezo wa ziara ya kusoma dua katika makaburi ya viongozi, waasisi wa Mapiduzi ya Zanzibar na Katibu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi ambapo kilele kitafanyika Aprili 7, 2025 Kisiwandui Wilaya ya Mjini, Unguja.