FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katika kuhakikisha msongamano wa wafungwa magerezani unapungua, Wizara ya Katiba na Sheria imeendeleza juhudi za kutekeleza haki jinai ikiwa ni pamoja na kutekeleza mapendekezo ya Tume kwa kuimarisha ulinzi wa watoa taarifa za uhalifu na mashahidi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro,alisema hayo mkoani Morogoro wakati wa mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Maafisa Sheria wa Jeshi la Magereza kuhusu huduma za msaada wa kisheria, mapokezi kwa wafungwa, adhabu mbadala, na matumizi ya mahakama mtandao.
Dkt Ndumbaro alisema kuwa jitihada mbalimbali zinafanywa na wizara yake, ikiwemo kutembelea magereza, ambazo zimeanza kuzaa matunda na takribani wafungwa 600 wameachiwa huru katika kipindi kifupi kutokana na maboresho ya mifumo ya haki jinai.
Alisema kuwa serikali kupitia Wizara hiyo imetoa seti 30 za vifaa vya TEHAMA kwa baadhi ya magereza nchini ili kurahisisha usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na kutatua changamoto ya kusafirisha wafungwa, hivyo kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati.
“Ni muhimu kuelewa kwamba mfumo wa mahakama mtandao si chaguo la mfungwa, bali ni uamuzi wa mahakama kuamua kesi ipi inasikilizwa kwa njia ya mtandao,” alisisitiza Dkt. Ndumbaro.
Aidha, alihimiza maafisa sheria hao kutumia siku hizo tano vya mafunzo kwa umakini mkubwa, wakitambua kuwa elimu watakayopata ni sehemu ya utekelezaji wa Mama Samia Legal Campaign inayolenga kuboresha upatikanaji wa haki nchini.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kuanzia Julai 2024 hadi Aprili 2025, watu 68 waliokuwa wamehukumiwa kifungo wakiwa na matatizo ya afya ya akili wameachiwa huru, hatua iliyoleta nafuu kubwa katika kupunguza idadi ya wafungwa.
Akizungumza katika hafla hiyo,Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji wa Haki Jane Lyimo alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kupunguza wafungwa na mahabusu magerezani, kuimarisha umahiri wa maafisa na kuboresha utendaji wa haki kwa wafungwa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dkt. Maduhu Kazi, alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha mlundikano wa wafungwa na mahabusu unapungua kwa kiasi kikubwa. “Kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2025, kumekuwa na wafungwa na mahabusu elfu 27, ikilinganishwa na elfu 32 mwaka 2021,” alisema.
Naye Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremia Matundu, alisema kuwa ndani ya Jeshi la Magereza kuna wanasheria zaidi ya 264, lakini ni 120 pekee waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo na kwamba ni muhimu kwa kuwaongezea ujuzi, kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Tunatarajia waliopata mafunzo haya watafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuwa walimu kwa wenzao ambao hawakushiriki,” alisema Matundu, na kuongeza kuwa jeshi la magereza litaendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa maafisa na wataalamu wake ili kwenda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia.
Amesema kwa sasa, jumla ya magereza 66 nchini yana huduma ya mahakama mtandao, lakini bado kuna wilaya 50 zisizo na magereza, hivyo kusababisha baadhi ya watuhumiwa kupelekwa katika wilaya jirani lakini mkakati wa Serikali ni kuongeza idadi ya magereza ili kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo chake.
Katika mafunzo hayo, washiriki watajifunza kuhusu adhabu mbadala, mabadiliko ya sheria, mapitio ya adhabu, matumizi ya mahakama mtandao, na utaratibu wa kutoa mapongezi kwa wafungwa pamoja na ushauri wa kisheria ndani ya magereza.
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya dhati ya kuboresha mfumo wa haki jinai, kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, na kuimarisha maisha ya wafungwa kwa njia ya kisasa na kisheria.