Na.Kulwa Meleka_DODOMA
LEO Mei 28,2025 Tanzania imeungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani, huku Wizara ya Afya ikizindua muongozo mpya wa hedhi salama pamoja na nyenzo zake.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto wa kike anaweza kutimiza ndoto zake bila vikwazo vinavyotokana na changamoto za hedhi.
Katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Otilia Gowele, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jensita Mhagama,ameeleza umuhimu wa siku hiyo.
Dkt. Gowele amesema kuwa changamoto za kiuchumi na kijamii zimekuwa zikisababisha asilimia 17 ya wasichana kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujistiri na maumivu makali wakati wa hedhi.
“Ni muhimu kwa jamii na wadau kutumia siku hii kama chachu ya kuimarisha juhudi za kuwawezesha wasichana kuhudhuria masomo bila vikwazo,” amesa Dkt. Gowele.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Joseph Birago, amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama yaliyoanzishwa mwaka 2015 yameleta mafanikio makubwa katika miaka kumi iliyopita.
Ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya hedhi, kupunguzwa kwa kodi ya bidhaa za hedhi, na uboreshaji wa miundombinu ya maji na usafi katika shule na jamii.
“Muongozo huu mpya wa hedhi salama unalenga kutoa mwongozo wa kisera na kimkakati ili kuhakikisha huduma bora za hedhi zinapatikana kwa wote,” ameongeza Dkt. Birago.
Naye mmoja wa wadau wa Jukwaa la Hedhi Salama alisisitiza umuhimu wa kuweka taulo za kike kama bidhaa muhimu ili zipatikane hospitalini kwa wanawake wenye bima ya afya.
Aidha, Wizara ya Afya imeweka mikakati madhubuti kama ujenzi wa vyumba vya kujistiri, usambazaji wa taulo za kike, na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu hedhi salama. Familia pia zimetakiwa kuhakikisha kuwa vifaa vya kujistiri vinapatikana kwa watoto wa kike majumbani mwao.
Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama yanahimiza jamii kuchukua hatua za msingi kuboresha huduma za hedhi na kuondoa imani potofu zinazokwamisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika shughuli za kijamii na kiuchumi.