Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amewataka Wenyeviti wa Bodi kushirikiana kwa karibu na menejimenti za taasisi zao kubadilika kimtazamo na kifikra kuhakikisha wanatekeleza mageuzi yatakayo leta tija katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya taasisi za umma.
Akizungumza katika kikao kazi na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo, Juni 2, 2025, kilichofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Bw. Mchechu amesema kuwa taasisi za umma 252 zinapaswa kufanya mabadiliko chanya katika mtazamo na fikra zao ili Watanzania wanufaike ipasavyo na maendeleo ya taifa.
“Muda umefika wa kuwa na mazingira bora ya usimamizi wa rasilimali ili ziweze kuleta manufaa kwa jamii. Taasisi lazima zijielekeze kwenye uzalishaji na ufanisi,” alisema.
Akitoa mifano, Bw. Mchechu amesema, “Leo kila wizara ipo Dodoma, lakini siyo wamiliki wa majengo yao. Mmiliki halali ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambaye anasimamia majengo yote ya serikali. Vivyo hivyo, licha ya Tanzania kuwa na rasilimali kama dhahabu, ni Tume ya Madini ya Taifa (STAMICO) iliyopewa jukumu la kusimamia leseni za madini. Kwa upande wa usafirishaji, serikali imewekeza matrilioni ya fedha TRC; Wizara ya Uchukuzi inasimamia kisera na utekelezaji, lakini mmiliki wa miundombinu hiyo ni TRC.”
Aidha, ameeleza kuwa tayari baadhi ya wenyeviti wa bodi na menejimenti wameanza kuelewa umuhimu wa kufanya mageuzi, na wengine wapo katika hatua mbalimbali za kutekeleza maboresho yanayolenga kuleta matokeo chanya.
Bw. Mchechu amesema kuwa kutokana na mikakati iliyopo, wanatarajia ndani ya miaka kadhaa kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika taasisi hizo.