Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni, ameibua hoja kuhusu ongezeko la wafanyabiashara kutoka mataifa ya Asia, hususan China, akisema kuwa pamoja na wingi wao, wamekuwa na tabia ya kukwepa kodi.
Akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mageni amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni pamoja na wa ndani wamekuwa wakikwepa kutumia mifumo ya kielektroniki ya malipo, na badala yake wanapendelea kufanya miamala kwa njia ya fedha taslimu (cash) ili kukwepa kodi.
“Hali hii si tu inakosesha serikali mapato, bali pia inaleta ushindani usio wa haki kwa wafanyabiashara wa ndani wanaolipa kodi kwa kufuata taratibu,” amesema Mageni.
Aidha, mbunge huyo ameitaka serikali kuimarisha udhibiti wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kuwa mifumo ya kielektroniki inatumika kikamilifu kwa wafanyabiashara wote bila ubaguzi, ili kuongeza mapato ya ndani na kulinda uchumi wa taifa.