KUSHOTO ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Mnenas Komba akiwa kabidhi madawati walimu wakuu kutoka shule tatu zilizokabidhiwa jumla ya madawati 150 kutoka NMB
KUSHOTO ni Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Roman Degeleki akimkabidhi madawati 150 Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Songea Mtela Mwampamba katika hafla iliyofanyika katika shule ya msingi Matimira
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Matimira wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa madawati 50 yaliyotolewa na NMB
…..
Benki ya NMB imeandika historia nyingine katika kuchangia maendeleo ya elimu nchini baada ya kukabidhi madawati 150 yenye thamani ya shilingi milioni 16.5 kwa shule tatu za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma.
Shule zilizofaidika na msaada huo ni Matimira, Magagura na Magima ambapo kila moja imepokea madawati 50, hatua inayolenga kupunguza uhaba mkubwa wa madawati unaokwamisha mazingira bora ya kujifunza.
Makabidhiano ya madawati hayo yalifanyika katika Shule ya Msingi Matimira, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali, jamii na wadau wa elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mtela Mwampamba aliipongeza NMB kwa moyo wa uzalendo na kugusa moja kwa moja changamoto za sekta ya elimu.
Alisema msaada huo ni mchango mkubwa katika kutatua tatizo la wanafunzi kuketi chini au kugawana madawati kwa zamu.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Roman Degeleki alisisitiza kuwa benki hiyo itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika maendeleo ya elimu, akibainisha kuwa kwa zaidi ya miaka minane sasa NMB imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya shughuli za kijamii kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii.
“Tunaamini elimu ni msingi wa kila maendeleo, na tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho,” alisema Degeleki.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matimira, Renista Vungu, alielezea faraja yake kwa msaada huo, akisema shule yao yenye wanafunzi 810 ilikuwa ikikumbwa na uhaba wa madawati 66.
“Kupatikana kwa madawati 50 kupitia NMB ni hatua kubwa kuelekea mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, hasa kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba wanaojifunza katika mazingira ya vijijini’’,alisema Vungu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe. Menans Komba, aliwataka walimu na wanafunzi kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa kwa uangalifu mkubwa.
Alisema kuwa rasilimali hizo zimetolewa kwa lengo la kuboresha safari ya kielimu kwa watoto wa Kitanzania, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuyalinda na kuyaendeleza kwa vizazi vijavyo.
Msaada huu kutoka Benki ya NMB si tu unajaza mapengo ya miundombinu ya elimu, bali pia ni uthibitisho wa namna taasisi binafsi zinavyoweza kushirikiana na serikali kuinua elimu ya msingi hasa maeneo ya vijijini.