

Dodoma, Novemba 5, 2025 — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuapisha BHamza Said Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla fupi iliyofanyika leo Ikulu Chamwino, jijini Dodoma.
Uapisho huo umefanyika kufuatia uteuzi alioufanya Rais Samia kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 59(1), ambayo inampa Rais mamlaka ya kumteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Rais Samia aliwataka viongozi wote kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo kwa maslahi mapana ya taifa.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Hamza Said Johari alishukuru kwa kuaminiwa na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria na haki kwa wote.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais – Ikulu, uteuzi wa Johari unalenga kuimarisha ufanisi wa sekta ya sheria nchini na kuhakikisha ushauri wa kisheria kwa Serikali unazingatia viwango vya juu vya kitaalamu na maadili ya utumishi wa umma.








