Na Mwaandishi Wetu Mtwara.
BODI ya Korosho Nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya Rhino Sports Talents Promotion imezindua vifaa vya mbio za korosho msimu wa nne kwa watoto, wazee na watu wa kawaida.
Mbio hizo za Korosho maarufu kama Korosho Marathon zinatarajiwa kufanyika Mkoani Mtwara tarehe 29,Novemba 2025.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vifaa hivyo na usajili kwa washiriki, Mkurugenzi wa Masoko na udhibiti ubora kutoka CBT Revelian Ngaiza, amesema Mbio za korosho msimu huu zitahusisha na mbio za watoto na wazee kwa lengo la kupanua wigo wa washiriki.
“Msimu wa nne wa mbio za korosho, mbali na zile mbio za kilomita Tano, kumi na 21, tutakuwa na mbio za kilomita 2.5 kwa watoto kuanzia miaka sita hadi 13, na kilomita 3 kwa wazee kuanzia miaka 60 hadi 95,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amepongeza waandaji wa mbio hizo huku akiwaomba wadau, wawekezaji kwenye tasnia ya korosho, na wazazi kujitokeza na watoto wao kushiriki katika mbio hizo.
Kwa mujibu wa CBT, lengo la korosho Marathon ni kutangaza fursa kwenye tasnia ya korosho kuhamasisha ulaji wa korosho, ubanguaji na kuongeza thamani katika zao la korosho.
Mratibu wa Mbio za Korosho kutoka Kampuni ya Rhino Sports Talents Promotion Nelson Mrashan amewaasa wazazi Mtwara na nje ya Mtwara kusajili watoto wao kushiriki mbio hizo ili kkuwajenga kifikra na kiafya kuwaandaa kuwa wakimbiaji wa baadae.
“Kama mnavyojua, riadhaa inaanzia miaka ya chini, nahamasisha wazazi kusajili watoto wao tuweze kupata wakimbiaji kufikia kiwango cha kimataifa,” amesema Mrashan.
Amesema usajili wa washiriki wakiwemo watoto na wazee utafanyika katika vituo vilivyowekwa Mtwara na kupitia mtandaoni.
Msemaji wa mbio za Korosho Mohammed Kemkem amesema zaidi ya watu 3000 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo huku akiwaomba wana riadha na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki.
Mbio za korosho msimu mwaka huu utatanguliwa na Maonesho ya shughuli na bidhaa mbalimbali za korosho ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Novemba.
Wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za fedha, Mashika na Taasisi za uwekezaji, biashara watashiriki kutangaza na kuonesha fursa kwenye tasnia ya korosho.














