KLABU ya Simba imetambia ushindi wake wa asilimia 100 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, ikisema ni ishara njema ya kwenda kutwaa taji hilo msimu huu, huku ikisema mkakati wao ni kushinda mechi tano za mwanzo.
Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, amesema jana, kitendo cha Simba kuwa timu pekee iliyoshinda michezo yote iliyocheza mpaka sasa kunawapa nguvu na morali ya kujituma zaidi kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji ili kuendelea kufanya vizuri.
Simba imecheza michezo mitatu ikishinda yote, ikiwa ni ushindi wa asilimia 100, kwani hakuna timu yoyote mpaka sasa zaidi yao, ambayo imeshinda michezo yote iliyocheza mpaka sasa.
Iliifunga Fountain Gate mabao 3-0, ikaichapa Namungo mabao 3-0, kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, Jumamosi iliyopita.
“Ukiona timu yoyote inaongoza ligi ujue hiyo timu imeizidi michezo Simba, tukikaa kwenye idadi sawa ya michezo sisi tutakuwa juu.
“Tumeanza vizuri ligi, tumeanza kwa ushindi wa asilimia 100, kampeni yetu ni kushinda michezo mitano ya mwanzo, tumeshinda mitatu bado miwili, tukimaliza hapo tunakuja awamu ya pili ya kushinda michezo mingine mitano.” alisema Ahmed.
Alisema wameridhishwa na mwanzo uliooneshwa na benchi ya ufundi lililo chini ya Dimitar Pantev raia wa Bulgaria, pamoja na uwezo unaooneshwa na wachezaji wao.
“Tumeridhika na kila idara, ukiangalia tumefunga mabao manane, tumeruhusu bao moja tu, tafsiri yake ni kwamba safu yetu ya ushambuliaji inafanya kazi yake vizuri, safu ya ulinzi nayo iko makini, tumeridhika, lakini bado tunaendelea kukiboresha kikosi ili tuwe imara zaidi kwa sababu hatujakutana na wapinzani wagumu zaidi,” alisema.
Kikosi cha timu hiyo kimerejea mazoezini jana kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua za makundi dhidi ya Atletico Petroleos de Luanda ya Angola unaotarajiwa kupigwa, Novemba 23, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Baada ya mechi dhidi ya JKT Tanzania kocha aliwapa mapumziko, akiwataka Jumanne kurejea mazoezi kwa wachezaji ambao hawapo kwenye vikosi vya timu za taifa. Simba ina wachezaji saba ambao wameitwa kwenda kutumikia vikosi vya timu za taifa,” alisema.
Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Yacoub Suleiman, Shomari Kapombe, Wilson Nangu, Selemani Mwalimu na Mourice Abraham ambao wamekwenda kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, huku Naby Camara, akienda kujiunga na Timu ya Taifa ya Guinea, pamoja na Steven Mukwala, aliyetwa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes.
Katika hatua nyingine Meneja Mkuu wa Klabu ya Simba, Dimitar Pantev, amesema mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda si mwepesi kama watu wanavyouchukulia.
Pantev, amesema kutokana na ratiba kubana, watakuwa na siku chache za kufanya maandalizi ya pamoja kwa wachezaji wake wote kabla ya kukabiliana na timu hiyo ya Angola.
“Tutakuwa na siku tatu au nne za maandalizi ya pamoja baada ya wachezaji waliopo kwenye timu za taifa kuungana nasi…, ukiangalia muda ni mchache na mchezo wa Ligi ya Mabingwa tena hatua ya makundi si michezo rahisi, tunahitaji kuunganisha nguvu zetu ili tufanye vizuri,” alisema Pantev.
The post WAKATI YANGA, AZAM WAKIJIKITA CAF ZAIDI…SIMBA WAJA NA JAMBO LA MECHI 5 LIGI KUU… appeared first on Soka La Bongo.



