
Kutokana na kuongezeka kwa changamoto za kisaikolojia miongoni mwa vijana hususan msongo wa mawazo, hofu, na kutokuwa na uelewa wa kina kuhusu afya ya akili vijana wa Kitanzania wameanza kuchukua nafasi yao katika kuunda suluhu za tatizo hili linalokua kwa kasi katika jamii.
Wikiendi hii, Tanzania Counseling Academy (TCA) ikishirikiana na Jamii Impact, waliandaa Klabu ya Mafunzo na Uimara wa Afya ya Akili (Mental Health Gym Club), programu jumuishi inayolenga kutoa eneo salama kwa vijana kukutana, kujadili, kujifunza na kupata msaada wa kisaikolojia kutoka kwa Wanasaikolojia na Wanasiihi ambao ni wanakundi-rika.
Lengo kuu la programu hii ni kuwasaidia vijana:
• Kujenga uelewa wa dhana ya afya ya akili
• Kutambua vyanzo vya msongo na wasiwasi
• Kupata msaada wa mwanzo wa kihisia kutoka kwa wanarika
• Kupanua uelewa wa waaashiriki kuhusu uthabiti (resilience) na mbinu za kujilinda kiakili.
Changamoto za Afya ya Akili ni Kubwa, Lakini Hatua Zinachukuliwa
Ingawa serikali imejitahidi kuweka mipango mbalimbali kukabiliana na tatizo la afya ya akili hasa kwa vijana; kama vile kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya ya Akili (National Mental Health Strategic Plan) unaotegemewa kuzinduliwa mwaka huu, kulingana na ripoti ya Africa Academy for Public Health (AAPH); mpango wenye lengo la kuimarisha huduma za kuzuia, kutambua na kutibu magonjwa ya akili, ikiwemo katika kundi la vijana; bado uhitaji ni mkubwa katika hili eneo kuliko huduma zilizopo.
Vijana ndio wahanga wakubwa zaidi wa changamoto hizi, na hivyo nguvu zao zinahitajika katika kutoa suluhu endelevu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), msongo wa mawazo na wasiwasi hugharimu uchumi wa dunia zaidi ya Dola za Marekani Trilioni 1 kila mwaka kutokana na kupungua kwa uzalishaji. Gharama za matibabu huongeza mzigo zaidi kwa familia na serikali. WHO inasisitiza kuwa:
“Afya ya akili si suala la kiafya pekee; ni suala la kiuchumi linaloweza kutishia ustawi na ukuaji endapo halitawekewa mkazo.”
Kwa Nini Mental Health Gym Club Ni Muhimu?
Kupitia ushirikiano wa TCA na Jamii Impact, klabu hii imewaleta vijana karibu na Wanasaikolojia, Wanasihi, na Wakufunzi wabobevu wa masuala ya afya ya akili, ambao wote ni vijana, hatua inayolenga kuongeza uelewa, kupunguza unyanyapaa, na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto kabla hazijafikia kiwango cha hatari. Hii ni sehemu ya kujenga uthabiti, kujenga msaada wa kijamii, na kupanua elimu ya afya ya akili kwa njia rafiki.

Mpango wa Baadaye
Klabu hii imelenga kufanyika kila mwezi, na kwa kadri rasilimali zinavyopatikana, TCA na Jamii Impact wanatarajia kupanua programu hii ili kuwafikia vijana wengi zaidi kutoka maeneo na makundi tofauti nchini.
Kwa pamoja, tunaunda kizazi chenye uelewa, kizazi imara, na kizazi kinachoweza kukabiliana na changamoto za afya ya akili bila hofu wala unyanyapaa.






