UONGOZI wa klabu ya Simba umemweka kwenye wakati mgumu kipa wao namba tatu, Hussein Abel, baada ya nyota huyo kuwasilisha ombi la kutaka kuondoka kutafuta changamoto mpya katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Abel amekuwa na hamu ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo limekuwa changamoto kutokana na ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zimeeleza kuwa Abel aliomba kuondoka ili kutafuta timu ambayo itampa muda zaidi uwanjani, lakini uongozi wa Simba umekataa ombi hilo.
Sababu kubwa ni kwamba klabu hiyo bado inamhitaji kutokana na mkataba alionao na umuhimu wake katika kipindi hiki kigumu cha msimu.
Simba imejikuta kwenye wakati mgumu katika idara ya ulinzi wa lango baada ya kipa wao namba moja, Moussa Camara, kupata majeraha.
Hali hiyo imeiacha timu ikiwa na makipa wawili tu, hivyo kumfanya Abel kuwa sehemu muhimu ya mipango ya benchi la ufundi hata kama hapo awali hakuwa chaguo la kwanza.
Kwa sasa, kipa anayepewa nafasi kubwa ya kuanza ni Yacoub Suleiman, ambaye ametwaa majukumu ya kuwa namba moja, huku Abel akipanda hadi nafasi ya kipa namba mbili.
Mabadiliko hayo yameongeza thamani ya uwepo wake ndani ya kikosi, jambo linalofanya uongozi kutotaka kumpoteza.
Chanzo kimesema kuwa mabadiliko hayo yamempa Abel fursa ya kuonekana muhimu na kuaminiwa na benchi la ufundi, hasa kutokana na mazingira ya ghafla yaliyotokea katika safu ya makipa.
Hata hivyo, licha ya kuhitajika, kipa huyo bado anadaiwa kutokuwa na msimamo wa kubaki na huenda akasubiri hadi dirisha kubwa la usajili kutafuta suluhisho.
Ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza kwa Abel kugomewa kuondoka. Katika dirisha dogo lililopita, Simba pia ilikataa ombi la KMC FC ambalo lilitaka kumsajili kwa mkopo, jambo linaloonyesha namna ambavyo klabu hiyo imeendelea kusisitiza umuhimu wake ndani ya kikosi.
The post ABEL APATA WAKATI MGUMU KWA SIMBA SC appeared first on Soka La Bongo.









