MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, ameibuka na kuikosoa kauli na kitendo cha Mwenyekiti wa Chama cha Vilabu Afrika (ACA), Hersi Said, akisema amechanganya masuala ya ushabiki na majukumu ya kiuongozi kwa njia iliyoikosea klabu ya Simba na kulichafua taswira ya nchi kimataifa.
Magori amesema kauli hiyo ilitolewa kufuatia hotuba ya Hersi, ambaye pia ni Rais wa Yanga, aliyopata fursa ya kuzungumza katika kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) nchini Qatar.
Katika hotuba hiyo, Hersi alizungumzia migogoro ya uongozi barani Afrika huku akionyesha picha za mashabiki wa Simba, jambo lililosababisha taharuki na tafsiri hasi.
Amesema ingawa hakutajwa jina la Simba moja kwa moja, kitendo cha kuonyesha picha za mashabiki wa klabu hiyo wakati wa kuzungumzia matatizo ya uongozi kilitoa ujumbe unaoelekeza lawama kwa Simba na Tanzania kwa ujumla. Kwa maoni yake, hilo halikuwa sahihi kwa kiongozi anayewakilisha vilabu vya Afrika.
“Kwa mtu anayesimama kama kiongozi wa vilabu Afrika na anatoka Tanzania, kuonyesha mbele ya Afrika na Dunia kwamba Tanzania ina matatizo, hasa kwa kutumia picha za mashabiki wa klabu bora nchini, kunatoa taswira isiyo sahihi,” alisema Magori.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ilipaswa kufikiriwa kwa kina kuhusu athari zake kwa nchi na soka la Tanzania.
Magori amesema kilichofanywa kinaonyesha kuchanganya ushabiki na uongozi. “Ameubeba ushabiki na kuupeleka sehemu ambayo haistahili. Uongozi mbaya haupimwi kwa matokeo ya uwanjani au malalamiko ya mashabiki baada ya timu kutofanya vizuri,” amesema .
Amefafanua uongozi mbovu unahusisha masuala kama rushwa, kukosekana kwa uwajibikaji, kutokuwa na uwazi katika maamuzi na ukiukwaji wa taratibu, siyo hisia za mashabiki au presha ya matokeo ya michezo.
Kwa mujibu wake, hayo ndiyo mambo yanapaswa kuzungumzwa kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa.
Magori ameongeza kuwa kiongozi anayepata nafasi ya kuzungumza mbele ya FIFA anatakiwa kuutetea na kuukuza mpira wa Tanzania, si kuutoa katika taswira hasi.
Ametolea mfano klabu kadhaa barani Afrika zenye matatizo makubwa ya uongozi ikiwamo kushindwa kulipa mishahara, kuvunja mikataba na kushtakiwa FIFA na wachezaji pamoja na makocha wao.
“Hayo ndiyo matatizo halisi ya uongozi barani Afrika yanayopaswa kupelekwa na kujadiliwa kwenye majukwaa kama yale, siyo kuhusisha mashabiki wa klabu au kuipa nchi taswira mbaya,” amesema Magori,
The post AMEUBEBA USHABIKI KUUPELEKA PASIPOSTAHILI, MAGOLI appeared first on Soka La Bongo.








