UONGOZI wa klabu ya Yanga unaendelea na jitihada zake za kuimarisha kikosi baada ya kupiga hodi klabu ya Singida Black Stars kwa lengo la kunasa saini ya kiungo Marouf Tchakei kwa mkopo katika dirisha dogo la usajili.
Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya Yanga na Singida Black Stars yamekuwa na mwitikio mzuri, huku pande zote mbili zikionesha utayari wa kufikia makubaliano yatakayomnufaisha mchezaji pamoja na klabu husika.
Imebainika kuwa majadiliano hayo kwa sasa yapo katika hatua za mwisho, ambapo kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa baadhi ya taratibu ndogo kabla ya mchezaji huyo kuruhusiwa kujiunga rasmi na kikosi cha Wananchi.
Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na dili hilo, viongozi wa Yanga wamethibitisha kuwa makubaliano yamefikia pazuri, na matarajio ni kwamba Tchakei atajiunga na klabu hiyo yenye maskani yake Jangwani ndani ya muda mfupi.
Nyota huyo tayari amepigiwa simu usiku na viongozi wa Yanga, wakimtaka kufika Jangwani kwa ajili ya kuanza taratibu za vipimo vya afya pamoja na zoezi la kupiga picha, hatua zitakazofungua mlango wa utambulisho wake rasmi.
Inaelezwa kuwa benchi la ufundi la Yanga linahitaji kiungo namba 10 mwenye uwezo mkubwa wa kupress na kuchezesha timu kwa kasi, ambapo jina la Marouf ndilo lililopitishwa mezani baada ya tathmini ya kina.
Tchakei ni mchezaji aliyewahi kuwindwa pia na Simba kipindi ambacho klabu ya Singida Black Stars ilikuwa ikitumia jina la Singida Big Stars, kabla ya kubadilisha jina, jambo linaloifanya dili hii kuwa na mvuto mkubwa katika ushindani wa klabu hizo kongwe.
The post JANGWANI KUMNASA NYOTA ALIYEWINDWA NA SIMBA appeared first on Soka La Bongo.








