WAKATI tetesi za kurejea ndani ya kikosi cha Simba zikizidi kushika kasi, kiungo wa Singida Black Stars, Clatous Chama, ameibua hisia nzito kwa mashabiki baada ya kujibu ujumbe wa shabiki unaoashiria kurejea kwake Msimbazi.
Chama amemjibu shabiki mmoja aliyemkaribisha kurejea Simba kwa maneno mafupi lakini yenye uzito, akisema “Mapema tu”, kauli iliyotafsiriwa na wengi kama ishara ya utayari wake wa kurejea ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Kwa kipindi cha usajili wa dirisha dogo kinachoendelea, jina la Chama limekuwa likitajwa mara kwa mara kuhusishwa na Simba, hasa katika mipango ya kuimarisha safu ya kiungo ya timu hiyo kwa ajili ya nusu ya pili ya msimu.
Tetesi hizo zimepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa Simba, ambao wamejitokeza kwa wingi kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za mchezaji huyo, wakimiminika na jumbe za upendo pamoja na kumkaribisha kurejea nyumbani.
Katika moja ya jumbe hizo, shabiki alimwandikia Chama kwa maneno, “Karibu Msimbazi mwamba”, ujumbe uliopata majibu ya haraka kutoka kwa mchezaji huyo na kuzua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki.
Kauli ya Chama imezidi kuwapa matumaini mashabiki wa Simba, ambao wanaamini uzoefu na ubora wake vinaweza kuipa timu nguvu mpya katika mbio za makombe ya ndani na kimataifa.
Ikumbukwe kuwa Clatous Chama aliwahi kuitumikia Simba kwa mafanikio makubwa kabla ya kusajiliwa na Yanga msimu uliopita, kisha kujiunga na Singida Black Stars msimu huu, huku sasa akiwa katikati ya uvumi wa kurejea tena Msimbazi.
The post CHAMA AFICHUA KUREJEA MSIMBAZI appeared first on Soka La Bongo.





