Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wakazi wa Kata ya Igandu wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya upandaji miti katika kipindi hiki cha msimu wa mvua, alipofanya ziara katika Kata hiyo kwa lengo la uzinduzi huo pamoja na kutembelea kituo cha Reli ya mwendo kasi Igandu Desemba 31, 2025
Habari – DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kikazi inayolenga kuzindua Kampeni ya Upandaji Miti katika Wilaya za Chamwino na Mpwapwa ikiwa ni baada ya uzinduzi rasmi wa Kampeni hiyo katika msimu huu wa mvua aliyoifanya Desemba 30, 2025 kwenye Hospitali ya Jiji la Dodoma ambapo sambamba na hilo, ametembelea na kukagua vituo vya Treni ya mwendo kasi vya Igandu na Gulwe.
Akiwa kwenye Shule ya sekondari Igandu ambapo alizindua zoezi la upandaji miti kwa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Senyamule amewasihi wananchi wa eneo hilo kupanda miti kwa wingi kwa kila kaya kwani Serikali imejipanga vyema kufikia azma ya kuikijanisha Dodoma na imezalisha miche ya kutosha kila mwananchi.
“Tumeanza kuzindua msimu wa kupanda miti kwa Mkoa wetu wa Dodoma, jana tumezindua pale Dodoma Jiji, leo tunazindua Chamwino na tumeelekeza kuanzia tarehe 01-07, kila mwananchi wa Dodoma, kila kaya ihakikishe inapanda miti na niwahakikishie, Serikali katika hilo imejipanga kupitia TFS kwani wana miche Milioni 1 ambayo imeshaoteshwa kwa kila mtu kupewa bure na kupanda”.
Aidha, ametoa wito kwa Wakurugenzi kuhakikisha miche inawafikia wananchi na kila kaya inapanda miti isiyopungua mitano nao, Maafisa mazingira wasimamie zoezi hilo ili liweze kufanikiwa ambapo kupitia Mpango wa Taifa wa Mazingira, Mkoa wa Dodoma umepangiwa kupanda miti 8,000,000 kwa mwaka hivyo, kila mkazi wa Dodoma atatakiwa kupanda miti mitatu.
Baadhi ya wanachi wa Kata ya Igandu, wamepongeza Kampeni hiyo ya upandaji miti na kusema itasaidia kuzuia mmomonyoko wa ardhi kutokana na mvua zinazoharibu mazingira sambamba na kupata faida zinazopatikana kutokana na miti kama vile kupata kivuli, matunda na faida nyingine za kiuchumi huku wakiwasihi wenzao kuitunza ili kunufaika nayo.
Kadhalika, akiwa kwenye kituo cha Treni ya mwendo kasi cha Igandu, Mhe. Senyamule amesema Treni hiyo ina kazi kuu mbili ambazo ni usafirishaji wa abiria na kutumika kwa shughuli za kiuchumi kama usafirishaji wa mazao kutoka hapo kuelekea maeneo mengine ya Tanzania hivyo amewasihi wananchi hao kujituma kwa kuzalisha mazao ya usafirishaji kwa wingi.
Licha ya hayo, Mhe. Senyamule, amezungumza na wananchi wa Kata ya Gulwe katika Wilaya ya Mpwapwa baada ya kuzindua Kampeni ya Upandaji miti kwenye shule ya msingi Gulwe na kuwasisitiza juu ya kuwapeleka watoto wote wenye sifa shule pindi mwaka mpya wa masomo 2026 utakapoanza kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa atakayeshindwa kutimiza hilo pasi na sababu za msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja akizungumza na wakazi wa Kata ya Igandu kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kuzungumza na kuzindua rasmi kampeni ya upandaji miti katika Wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa vituo vya reli ya mwendo kasi Desemba 31, 2025
Baadhi ya viongozi wa Kata ya Igandu na walioongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwenye uzinduzi wa Kampeni ya upandaji miti katika Wilaya ya Chamwino wakimsikiliza wakati akizungumza na wakazi wa Kata hiyo kwenye ziara yake iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa vituo vya Reli ya mwendo kasi Desemba 31, 2025






