Na Ibrahim Dunia Maelezo 11.01.2026
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Mhe. Shariff Ali Shariff amesema Serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu hiyo katika maeneo mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu bora na mazingira wezeshi ya kujifunzia.
Mhe. Shariff ameyasema hayo wakati akifungua Skuli ya Kitope, kwa niaba ya skuli za Kibuyuni, Kinyasini, Donge, Koani, Jumbi, Fuoni Kipungani, Kizimkazi na Kitogani ikiwa ni muendelezo mwa shamrashamra za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi.
Amesema uimarishaji wa miundombinu ya Elimu ni kuweka mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi sambamba na kuengeza ufaulu kwani miundombinu hizo zinavifaa bora ambavyo vinaenda sambamba na mabadiliko ya tehama.
Aidha, Mhe Shariff amewataka Wazazi na Walezi kuhakikisha Wanafunzi wanapata mahitaji muhimu ya Skuli pamoja na kuwajengea maadili mema ili waweze kuwa raia wema wenye mchango chanya katika maendeleo ya Taifa.
Vilevile amesisitiza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yanahitaji ushirikiano wa wananchi katika kuitunza na kuilinda kwa maslahi ya taifa la leo na taifa la kesho.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdulla Said, amesema kuwa skuli nane kati ya hizo zimejengwa na Kikosi cha KMKM Marine chini ya usimamizi wa Mshauri Elekezi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), huku skuli ya maandalizi ya Fuoni Kipungani ikijengwa na Kikosi cha Chuo cha Mafunzo na kusimamiwa na Mshauri Elekezi wa AE&Q Consulting Company.
Ameongeza kuwa kila skuli ina jumla ya madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 180 kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa pamoja na kila skuli ina vyoo 12, ofisi ya Mwalimu Mkuu, ofisi ya walimu, ukumbi wa kula pamoja na jiko.
Ujenzi wa Skuli zote tisa umegharimu Shilingi Bilioni 3.6 kwa mujibu wa mkataba, ambapo kila Skuli moja imegharimu shilingi milioni 400 ambapo ujenzi wa skuli hizo za maandalizi ulianza mwezi Agosti 2024 na kukamilika mwezi Oktoba 2025.






