Na.Sophia Kingimali.
Mradi wa ujenzi wa matangi 15 ya kuhifadhia mafuta wenye thamani ya Sh bilioni 678.6 umeelezwa kuwa kichocheo kipya cha mapinduzi ya nishati na biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuweka jiwe la msingi kuashiria mwanzo rasmi wa utekelezaji wake.
Akizungumza Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, alisema mradi huo utakaotekelezwa katika eneo la Kigamboni Mnadani ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uhifadhi na usambazaji wa mafuta kwa nchi za ukanda huu.
Amesema badala ya kuangalia tu upanuzi wa bandari, Serikali imeamua kuwekeza kimkakati katika miundombinu ya kuhifadhi nishati ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kupunguza gharama za uagizaji na usambazaji wa mafuta nchini na nje ya mipaka.
Aidha Profesa Mbarawa,ameongeza kuwa matangi hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya mita za ujazo 378,000 za mafuta, hatua itakayosaidia kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku tatu pekee, hivyo kuongeza mzunguko wa huduma na mapato.
Amefafanua kuwa ongezeko hilo la uwezo wa uhifadhi litaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuvutia zaidi meli kubwa za mafuta na wawekezaji wa kimataifa, sambamba na kuimarisha usalama wa nishati nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa akiba ya kutosha wakati wote.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alieleza kuwa maboresho hayo yanaenda sambamba na ujenzi wa magati mapya na kuimarishwa kwa miundombinu mingine ya bandari, hatua itakayoongeza uwezo wa kupokea hadi tani milioni 60 za mizigo kwa mwaka pindi miradi itakapokamilika.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia takribani tani milioni 19.9 za mizigo, huku matarajio ya Serikali yakiwa kufikia tani milioni 40 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26 kutokana na maboresho yanayoendelea.
Aidha, Serikali imeunganisha mkakati huo na uimarishaji wa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway, lengo likiwa kusafirisha kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mizigo yote kupitia reli badala ya barabara ili kupunguza msongamano na ajali.
Profesa Mbarawa alisisitiza kuwa sekta ya uchukuzi inaendelea kuwa mhimili mkuu wa uchumi wa taifa kwa kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya mapato ya Serikali kupitia kodi za forodha na kuiingizia nchi wastani wa Dola za Marekani milioni 2.48 kwa mwaka kutoka nchi jirani, huku mradi wa matangi ya mafuta ukitarajiwa kuongeza zaidi mchango huo katika miaka ijayo.






