Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Christian Nyakizee akizungumza leo Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufuatilia matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi miwili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara za Nyaishozi, zilizopo Kata ya Bunju, yenye thamani ya Shilingi 5,093,574,007.66.
Akizungumza leo Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Christian Nyakizee, amesema kuwa katika ufuatiliaji wa miradi hiyo imebainika kuchelewa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo hali ya hewa, kuchelewa kwa malipo, pamoja na ombi la msamaha wa kodi katika mradi kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo mabadiliko ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
“Baada ya kubaini hayo, ofisi ilifanya kikao kazi na watekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inakamilika ndani ya muda wa nyongeza waliopatiwa kwa kuzingatia ubora, wakiwemo wakandarasi, washauri na wasimamizi wa miradi hiyo ili kuendana na thamani ya fedha,” amesema Nyakizee.
Amesema kuwa katika hatua nyingine, wamefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali waliokutana nao, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Nyakizee amesema hatua hiyo imepunguza malalamiko ya vitendo vya rushwa katika ngazi za mitaa, vijiji na kata, na kuwajengea ujasiri na uwajibikaji wanafunzi waliopo katika klabu za wapinga rushwa.
“Makundi ya wananchi tuliyoyafikia ni watumishi wa umma, asasi za kiraia, wanafunzi, VICOBA, viongozi wa masoko, viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, pamoja na maafisa usafirishaji wa bodaboda na bajaji,” amesema Nyakizee.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa wamepokea malalamiko 72 katika kipindi hicho, ambapo malalamiko 25 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 47 hayakuhusu vitendo vya rushwa. Kati ya malalamiko 25 yaliyohusu rushwa, uchunguzi wake unaendelea na upo katika hatua mbalimbali.
Amesema kuwa malalamiko 45 ambayo hayakuhusu rushwa, walalamikaji walishauriwa ipasavyo.
Aidha, kesi 19 zinaendelea mahakamani, ambapo kati ya hizo, kesi mpya moja ilifunguliwa na kesi nne zilitolewa maamuzi, huku Jamhuri ikishinda kesi zote nne.
Nyakizee amefafanua kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu wameweka mikakati ya kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo, kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu kuzuia rushwa kwenye miradi hiyo, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Programu ya TAKUKURU Rafiki.
Ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo hivyo katika maeneo yao. Aidha, amewataka kupiga simu namba 113 bure au kuwasiliana na ofisi ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa kwa taarifa zaidi.



