……..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imezitaka Mamlaka wanazozisimamia kutangaza mikataba ya huduma kwa wateja ili wananchi waweze kujua haki na wajibu wao.
Rai hiyo imetolewa Leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja.
Mhina amesema pamoja na kutoa rai hiyo, pia ameeleza kuwa watapita kwa wananchi kwaajili ya kuwaeleza mikataba ya huduma kwa wateja waliyokuwanayo watoa huduma wao.
“Wananchi wanapokosa huduma na mamlaka husika imeshindwa kuwajibika ipasavyo basi kwakupitia mikataba ya huduma kwa wateja wananchi waweze kufatilia haki zao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwetu kwa kigezo cha mamlaka husika imeshindwa kutekeleza mkataba wake wa huduma kwa wateja”, amesema Mhina.
Ameeleza kuwa wamepewa mamlaka ya kusimamia mikataba ya huduma kwa wateja ambapo kwenye mkataba huo unaelezea haki na wajibu wa mtoa huduma na mteja.
Amesema EWURA Kanda ya Ziwa wameiyadhimisha wiki hiyo kwakukutana na wateja wao kwa ajili ya kuwapa elimu.










