Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimefika mezani kwetu, wawakilishi wa kiungo wa Yanga SC, Aziz Andabwile, wamefungua rasmi kesi TFF wakidai fedha za usajili (signing fees) ambazo hadi sasa hazijalipwa na klabu hiyo.
Kesi hiyo itasikilizwa Alhamisi, Novemba 13, 2025, katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Meneja wa Andabwile, Bw. Hillary, amethibitisha kupitia kituo cha CROWN SPORTS kuwa ni kweli mchezaji huyo hajalipwa fedha zake tangu aliposaini mkataba wake na Yanga SC.
“Ni kweli kabisa, Aziz hajalipwa fedha zake za usajili. Tumefika hatua ya kisheria, na kesi yetu itasikilizwa kesho TFF,” amesema Bw. Hillary.
Tukio hili limeibua maswali mengi kuhusu uaminifu wa Yanga SC katika masuala ya mikataba na malipo, klabu ambayo imekuwa ikihusishwa mara kwa mara na malalamiko ya wachezaji wanaodai fedha zao.
Mashabiki na wadau wa soka wameonyesha kukerwa na tabia hii ya “kudaiwa kila mara” ya klabu kongwe kama Yanga, wakitaka TFF ichukue hatua kali kuhakikisha wachezaji wanalipwa haki zao kwa wakati.
“Ni aibu kwa klabu kubwa kama Yanga kuendelea na tabia za kudaiwa. Hawa wachezaji wanatumikia timu, wanastahili kulipwa kwa haki zao,” ameandika shabiki mmoja mkongwe wa Yanga, Esir Said .
The post Mchezaji Andabwile na Yanga Kimenuka, Wakokotana Hadi TFF Kushtakiana appeared first on SOKA TANZANIA.



