Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkesha mkubwa wa kuliombea Taifa, utakaofanyika Ijumaa hii, Machi 14, 2025, katika ukumbi wa Ubungo Plaza.
Lengo la mkesha huo ni kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 ili ufanyike kwa amani na utulivu.
Mkesha huo umeandaliwa na Kiongozi wa Kanisa la Heavenly Image Manifest (HIM) chini ya Nabii Edmund Mystic, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, utakaonza saa 2:00 na kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Machi 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Nabii Edmund, alisema mkesha huo awali ulipangwa kufanyika Februari 28, mwaka huu na ukasogezwa mbele hadi Ijumaa hii.
Nabii Edmund alisema kwa Tanzania mwaka 2025 ni muhimu kwa Taifa kwasababu ya tukio kubwa la uchaguzi mkuu ambao utaamua hatma ya nchi kwenye utawala wa viongozi.
Alisema kanisa lina nafasi ya kulibeba Taifa kwa namna moja na nyingine kwa kufanya maombi hivyo yatahusisha pia kumwombea Rais Samia kwasababu yeye ni mtawala na amebeba hatima kubwa ya Watanzania.
Alisema hawawezi kuombea serikali wanayoitazamia kwenye uchaguzi ujao pasipo kuanza na serikali iliyopo madarakani hivyo ni lazima kumwombea Rais Samia ambaye Mungu alimuweka kwenye kiti cha urais.
“Kila Mtanzania ana nafasi ya kusimama na kuiombea Taifa la Tanzania kwa imani yake na kile Mungu atakachompa kuombea kwa sababu biblia imesema.
“Habari ya kuombea Tanzania ni suala nyeti ambalo Mungu anaenda kuikumbuka nchi na kuirehemu, kama kuna makosa tumefanya alafu tukasimama kuomba rehema kwa Tanzania Mungu ana uwezo wa kufanya kitu, maombi ni kitendo cha unyenyekevu na tuna muhitaji Mungu aingilie kati katika haya,”alisema Nabii Edmund.
Alisema yanayoendelea nchini Congo si kwamba wananchi wake wanapenda, hivyo ni wajibu wa Watanzania na waombaji kuliweka Taifa mikononi mwa Mungu kwa maombi ili aghairi mabaya yote.
“Hatupendi kuona Rais mwingine anafia madarakani na badala yake kama watumishi wa Mungu yapo yale ambayo Mungu anasema na sisi, tusiishie kuyasema tu bali tuyafanyie kazi kwa njia ya maombo,” alisema.
Nabii Edmund, alisema kuwa yapo mambo yanaonekana katika ulimwengu wa kiroho ambayo wakati mwingine yanaweza kuwa mazuri au mabaya hivyo kama watumishi wa Mungu kazi yao kubwa ni kuyaombea mambo yote ili Taifa liendelee kuwa salama.
Alisema wanasiasa watakaogombea wanapaswa kuzingatia uchaguzi unaosimamia haki na sheria ambazo zimeweka nchini.
Aidha, Edmund alisema kuwa waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili pamoja na watumishi wa Mungu kutoka makanisa mbalimbali nchini watakuwapo.
Aliwataja baadhi ya waimbaji watakaoishiriki ni Upendo Nkone, Beatrice Mwaipaja, John Lisu, Kwaya ya Uinjilisti KKKT Kijitonyama na Kwaya ya Ufunuo.