Na Mohamed Saif, Ruvuma
Serikali
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleleza mradi wa shilingi
bilioni 14.56 wa kusambaza umeme katika vitongoji 135 Mkoani Ruvuma
utakaonufaisha Kaya 4,455 mkoani humo.
Mhandisi
Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu
amebainisha hayo Septemba 30, 2024 Mkoani Ruvuma mbele ya Mkuu wa Mkoa huo,
Mhe. Kanali Ahmed Ahmed wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni
ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya CCC International Nigeria LTD.
“Katika
kuhakikisha maendeleo yanafika kote nchini, Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeidhinisha kiasi cha
shilingi bilioni 14.56 kitumike kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika
vitongoji 135 Mkoani hapa,” alisema Mhandisi Nagu.
Akizungumza
wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed
Ahmed aliipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia kwa
vitendo na alimsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati na
kwa ubora unaotakiwa.
Kanali
Ahmed alitoa wito kwa wananchi maeneo ya miradi kuwa waadilifu kwa kulinda na
kutunza miundombinu ya umeme na aliwasihi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili
kumrahisishia utekelezaji.
“Mkandarasi
hakikisha unawashirikisha wananchi, wawe na taarifa sahihi na hii itakusaidia
kupata ushirikiano kutoka kwao lakini pia ofisi yetu ipo wazi na tutakupatia
ushirikiano utakaouhitaji,” alisema Kanal Ahmed.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme vitongojini, Mhandisi Nagu alisema kati
ya vitongoji 3,693 vilivyopo Mkoani humo, vitongoji 1,973 vimefikishiwa umeme
ambayo ni sawa na asilimia 53 na kwamba vitongoji 135 ambavyo vitapata umeme kupitia
mradi huo na kuongeza idadi ya vitongoji
vyenye umeme katika Mkoa wa Ruvuma.
Aidha,
alibainisha kuwa mradi huo ambao mkandarasi wake ametambulishwa hivi leo,
utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na hivyo kukamilika ifikapo Septemba 2026 na
kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kupatiwa umeme kulingana na
upatikanaji wa fedha.
Mhandisi
Nagu alisema mradi utatekelezwa katika majimbo Tisa katika wilaya za Songea,
Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru na kwamba katika kila Jimbo Vitongoji 15
vitanufaika.
Kuhusiana
na hali ya upatikanaji wa umeme vijijini kwa ujumla katika Mkoa huo, Mhandisi
Nagu alisema Mkoa wa Ruvuma unajumla ya vijiji 554 ambavyo alibainisha hadi
hivi sasa vyote vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 100.
“Serikali
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi
mbalimbali ya umeme vijijini nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu
Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha
miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili iweze
kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa,” alisema.
Alimuhakikishia
Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Wakala umejipanga vyema kuhakikisha umeme unafika kwenye
vijiji vyote kote nchini na kwamba baadhi ya Mikoa ikiwemo Ruvuma vijiji vyote
tayari vimefikiwa na sasa unasambazwa vitongojini.
Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme Mkoani Ruvuma kwa Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Ahmed Septemba 30, 2024 wakati wa kumtambulisha
Mkandarasi Kampuni ya CCC Intrnational Nigeria Ltd (hayupo pichani)
anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vitongojini mkoani humo.
Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Ahmed (wanne kushoto) katika picha ya pamoja na
ujumbe kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) Mkoa wa Ruvuma wakati wa hafla ya kumtambulisha Mkandarasi
anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vitongojini mkoani humo, CCC
International Nigeria Ltd aliyewakilishwa na Mhandisi Li Rongqing (wa tatu
kushoto).