MSAIDIZI wa mama lishe soko la samaki Malindi, Khadija Nassor, akitoa maoni yake juu ya kutumikishwa kwa watoto wakati Tume ya haki za binaadamu na utawala bora ikichukua maoni ya wadau kuelekea kuandaa mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na Biashara.
SHEHA wa Shehia ya Malindi, akitoa maoni yake juu ya kutumikishwa kwa watoto wakati Tume ya haki za binaadamu na utawala bora ikikusanyaji maoni ya wadau kuelekea kuandaa mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na Biashara.
(PICHA NA FAUZIA MUSSA).
NA FAUZIA MUSSA
WAFANYABIASHA na wadau wa uchumi wa buluu wameishauri Tume ya haki za Binaadamu na utawala bora (THBUB), kulipa uzito suala la utumikishwaji wa watoto wakati wa kuandaa Mpango kazi wa haki za binaadamu na Biashara ili kukomesha vitendo hivyo kwa maslahi ya watoto na maendeleo ya Taifa.
Wadau hao walitoa rai hiyo katika soko la samaki Malindi Mjini Unguja, wakati wakitoa maoni yao kwa Tume hiyo ikiwa ni awamu ya pili ya kuchukua maoni ya wadau katika maandalizi ya mpangokazi wa Kitaifa wa haki za binaadamu na biashara.
Walisema licha ya kuwa katika soko hilo hakuna utumikishwaji wa watoto unaonekana lakini bado baadhi ya maeneo matukio kama hayo yapo na yanaendelea kuwaathiri watoto na taifa.
“uzowefu unaonesha kuwa watoto wengi wanaotumikishwa huacha kabisa masomo yao na wanaoendelea hupata matokeo mabaya katika masomo yao, hali hii itatupelekea kuwa na Vijana tegemezi ndani ya jamii kama halikudhibitiwa. ” walisema wadau hao
Waliongeza kwa kusema kuwa hali hiyo inasababishwa na baadhi ya watoto hao kuishi karibu na maeneo ya bahari pamoja na haliduni za maisha kwa baadhi ya jamii na familia zao.
Aidha walieleza kuwa malezi ya mzazi mmoja hasa yanayosababishwa na kuachana kwa wazazi hao kunachangia baadhi ya watoto kujiingiza katika biashara kinyume na sheria.
” watoto hawa huingia katika biashara kwa sababu ya wazazi au walezi kukosa kipato cha kuwahudumia ipasavyo hali inayowasukuma kuanza kujipanga kupambana na maisha kutokana na kuona familia zao hazina uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na hata baadae.” alisema msaidizi wa mama lishe soko la samaki Malindi Khadija Nassor.
Hivyo aliishauri Tume ya haki za binaadamu na Utawala Bora kutoa elimu Kwa jamii juu ya Athari za utumikishwaji wa watoto na kuwaomba wazazi kutopeana talaka kiholela, pamoja na kuchukua juhudi za kutimiza mahitaji ya watoto ili kuwapa fursa ya kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu.
Kwaupaande wake Naibu Katibu mtendaji tume hiyo Ofisi ya Zanzibar Juma Msafiri Karibona alisema wakati tume hiyo ikiandaa Mpango kazi huo itazingatia maoni yaliyotolewa na wadau ili kupata Mpangokazi uliozingatia maslahi ya jamii.
Alifahamisha kuwa katika kuandaa mpangokazi huo watahakikisha wanawafikia wadau wote waliokusudiwa ili kupata mpango shirikishi kwa maslahi ya Taifa.
katika kupata maoni juu ya utumikishwaji wa watoto tume hiyo ilikutana na wafanyabiashara na wadau wa uchumi wa buluu katika soko la samaki ngalawa, malindi na fumba kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na kuchukuwa maoni katika maeneo ya wadau kama hao walio katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja.