Wataalamu na taasisi zinazohusika na utafiti wa misitu wametakiwa kutumia ujuzi wao kufanya tafiti ambazo zitaisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzisha stoo ya mbegu za muda mrefu (Genebank) kwa miti ya asili. Hatua hii inalenga kukabiliana na hatari ya kupotea kwa vizazi vya miti ya asili na mimea pori kutokana na uharibifu unaoendelea wa misitu ya asili na matumizi yasiyo endelevu ya mazao ya misitu.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Kitivo cha Mafunzo ya Misitu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Biolojia ya Mbegu za Miti wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Fandey H. Mashimba, alionya kuwa uharibifu wa misitu unatishia kutoweka kwa vizazi vya miti ya asili. Alisema mimea takribani aina 314 iko katika hatari ya kutoweka duniani kulingana na Shirika la Uhifadhi la Kimataifa (IUCN).
Mashimba alitoa wito kwa wataalamu wa SUA na wadau wengine kushawishi mamlaka kuona umuhimu wa kuanzisha Genebank ya kitaifa. Alisema nchi nyingi, kama Uingereza, zina stoo za mbegu za miti kupitia taasisi kama Millenium Seed Bank Partnership. “Hifadhi ya mbegu za muda mrefu inaweza kuwa suluhisho la kudumu katika kuhifadhi vizazi vya miti hiyo pamoja na mingine,” alisisitiza.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kudhibiti uagizaji wa mbegu za miti kutoka nje ya nchi, akibainisha hatari ya kuingiza magonjwa yanayoweza kuathiri mashamba ya miti ya serikali na misitu kwa ujumla. Sheria ya sasa inathibiti mbegu za kilimo pekee, na hivyo kuwepo ombwe katika udhibiti wa mbegu za miti.
Mashimba pia alionya kuhusu matumizi ya mimea vamizi kama muaradi (Mutingia calabura), ambayo imeanza kuleta athari jijini Dar es Salaam kwa kuongezeka kwa idadi ya popo wanaotumia matunda yake kama chakula.
Dkt. Fecian Kilahama, Mkurugenzi Mstaafu wa Misitu na Nyuki, aliunga mkono wito wa Mashimba kwa kuhimiza kuwa ushauri wa wataalamu wa misitu unapaswa kuheshimiwa na wanasiasa. Alisema misitu ya asili ni muhimu kwa sekta nyingine, hususan katika kutoa maji kwa mito takribani 90 nchini Tanzania. Alihimiza mapato yatokanayo na matumizi ya maji yaelekezwe kwenye kuhifadhi misitu.
Washiriki wa maadhimisho hayo walikiri kuwa yamewasaidia kuongeza uelewa wa umuhimu wa kutunza misitu ya asili kwa ajili ya vizazi vijavyo.