Na. Damian Kunambi, Njombe.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza mkakati wa kuingia makubaliano na sekta binafsi za ufundi Ili kuboresha elimu ya ufundi na kuwafanya wanafunzi kupata maarifa yaliyo na tija zaidi.
Hayo ameyasema Wilayani Ludewa Mkoani Njombe alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo chuo cha mafunzo ya ufundi (VETA) na kuongeza kuwa mafundi binafsi watakaoonekana kuwa na ujuzi na ubunifu wataazimwa ardhi ya kuweka kiwanda jirani na chuo ambacho kitatumika kufundishia wanafunzi hao.
“Tutatafuta watu wajuzi wa ufundi kama uselemala, ushonaji na ufundi mwingineo ambapo wanafunzi wataenda kufanya mazoezi kwenye hicho kiwanda na vitu vitakavyozalishwa pale ataviuza yeye mwenyewe hivyo haita hitajika kulipwa na serikali malipo yoyote kwakuwa atakuwa amesaidiwa nguvu kazi”.
Joseph Kama ni bunge wa Jimbo la Ludewa alitumia fursa hiyo kwa kuwasilisha ombi la kumaliziwa kwa kituo cha Afya ambacho kumekuwa pagale kwa miaka mingi Ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwani chuo hicho kitakusanya wanafunzi zaidi ya elfu moja hivyo huduma ya afya ni muhimu kwao.
“Mheshimiwa Waziri pale unapokatisha Kona yakuja kwenye chuo hiki Cha VETA kuna jengo la kituo cha afya ambacho bado hakijamaliziwa, hivyo kwakuwa ziara yako inahusisha utekelezaji wa miradi ya aina zote naomba nikuwasilishie ombi la kupata fedha za kimalizia ujenzi wa kituo hiki kwani Kata hii ya Lugarawa kupitia chuo hiki kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu ambao watahitaji kupata huduma ya afya”.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas amesema chuo hicho kina umuhimu mkubwa kwa jamii kwani Wilaya hiyo inaelekea katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma hivyo endapo vijana watapata elimu ya vitendo itawasaidia kupata ajira katika viwanda na mradi hiyo.
Ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa miradi hiyo mikubwa lakini pia wanaludewa ni wakulima wakubwa wa mazao ya mbao hivyo elimu ya ufundi itakayotewa chuoni hapo utasaidia vijana kujiajiri katika utengezaji Samani mbambimbali pamoja na vitu vingine.
Katika ziara hiyo Waziri Prof. Mkenda pia amezindua nyumba pacha ya walimu katika shule ya sekondari Lobonde, amekagua vyumba vitano vya Madara na matundu matano ya vyoo.