Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kuendelea kutafuta maoni kuhusu sheria inayoisimamia Mfuko huo ili kuboresha utoaji wa fidia kwa wafanyakazi.
Jaji Mkuu ametoa wito huo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi baina ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) hivi karibuni.
Pamoja na pongezi hizo, Prof. Juma amewahimiza Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania kuendelea kutoa ushauri wa kisheria utakaosaidia kufanyika kwa maboresho ya sheria Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na hivyo kuongeza tija na ufanisi kwenye mnyororo wa utoaji haki kwa wafanyakazi wanaopata madhila kutokana na kazi.
“Tufahamu kwamba, ushirikiano kati ya Mahakama, Mfuko wa Fidia, na wadau wote katika mnyororo wa haki za wafanyakazi nchini ni sehemu ya Malengo ya Kikatiba ya Ustawi ya Jamii unaolenga kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinazingatiwa na kulindwa ipasavyo,” ameongeza Jaji Mkuu.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa kufunga kikaokazi hicho amewahakikishia waheshimiwa Majaji hao kuwa mapendekezo wanayotoa ya uboreshaji wa sheria hizo yanapokelewa na kufanyiwa kazi.
“Eneo ambalo tunatamani zaidi kuendelea kupata mapendekezo yenu ni juu ya namna bora ya kuwahimiza waajiri ambao hawajajisajili WCF na kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kufanya hivyo bila kulazimishwa. Eneo hili ni muhimu sana kwani waajiri wasiotekeleza Sheria hiyo ya Fidia kwa Wafanyakazi wanakwamisha jitihada za Serikali katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanakuwa na uhakika wa kipato pale wanapopata ulemavu kutokana na ajali au magonjwa yanayotokana na kazi, au kwa wategemezi wao iwapo mfanyakazi atafariki kwa ajali au ugonjwa unaotokana na kazi,’ alisema Waziri Kikwete.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kwamba ushirikiano baina ya Mfuko huo na Mahakama ya Tanzania umechangia katika maboresho kadhaa kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ambapo pia michango ya waheshimiwa Majaji imehusika.
“WCF imeshiriki katika ufuatiliaji wa uboreshaji wa sheria mbalimbali kuhusu fidia ili kuongeza ustawi kwa wafanyakazi na familia zao na hatimaye kutunza nguvu kazi na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla,”alisema Dkt. Mduma
Kikaokazi hicho pia kilihudhuriwa na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu, Manaibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani, Watendaji wa Mahakama, Makamishna wa Kazi kutoka bara na Zanzibar, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pamoja na Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii.
The post Majaji Mahakama ya Rufani watoa nasaha kuzidi kuijenga WCF first appeared on Millard Ayo.