Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi, amesema Serikali itaendelea kuheshimu misingi iliyowekwa na vyama vya siasa katika kujenga amani na utulivu kwa watanzania wote.
Kauli hiyo ameitoa tarehe 8/10/2024 Jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kutembelea Makao Makuu ya ofisi za vyama vya UDP, NCCR MAGEUZI, CUF na NLD, ambapo amepata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa vyama hivyo.
Ameeleza kwamba tangu mfumo wa vyama vingi umeanza nchini vyama vya Siasa kwa kushirikiana na chama tawala vimekuwa mhimili wa kujenga amani na umoja, hivyo akawapongeza kwa kazi nzuri ya uzalendo wanayofanya.
“Niombe viongozi wa vyama, mhimize wananchi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ndani ya demokrasia ya vyama mnaweka wagombea ili washindane na vyama vingine kupata viongozi,” alisema Waziri Lukuvi
Aidha alisema Serikali itahakikisha matangazo yote ya vijiji yanawekwa kwenye tovouti za Serikali ili wananchi wafahamu vijiji, vitongoji na mitaa inayogombaniwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha UDP Mhe. John Cheyo amemshukuru Waziri wa Nchi kwa kufanya ziara katika ofisi za makao makuu ya vyama kwasababu imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kutekeleza falsafa ya 4R.
Mhe. Cheyo amesema “sisi kama wadau wa siasa tunataka kushiriki katika kuona nchi inatawalika kwa amani na kuchagiza maendeleo makubwa”
The post Serikali inaheshimu misingi ya vyama vya siasa katika kujenga amani :Waziri Lukuvi first appeared on Millard Ayo.