Na Sophia Kingimali
Kampuni inayojihusisha na uokoaji katika vivutio vya utalii nchini, Kili MediAir Aviation, imepanga kuzindua kifurushi kipya cha huduma kinacholenga kusaidia watalii wa ndani na nje kufurahia vivutio vya utalii, hususan Mlima Kilimanjaro, bila kuhofia usalama wa afya zao.
Daktari wa Uokozi wa Kampuni hiyo, Jimmy Daniel, alibainisha hayo leo, Oktoba 12, 2024, wakati akizungumza kwenye Maonyesho ya Nane ya S!TE yanayoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Akielezea mpango huo, Dk. Daniel alisema kuwa kifurushi hicho kinalenga kusaidia watalii ambao wanakumbwa na changamoto kama maradhi au umri kuwa na nafasi ya kutembelea mlima kwa usalama kwa kutumia helikopta.
“Watalii wengi wangependa kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini umri au hali zao za kiafya zinakuwa kikwazo. Kili MediAir tumekuja na huduma mpya inayowawezesha kufurahia safari kwa kutumia helikopta, kufika maeneo ambayo si rahisi kufikiwa na mtu wa kawaida,” alisema Dk. Daniel.
Aliendelea kufafanua kuwa watalii watakaotumia huduma hiyo watapewa daktari na mhudumu maalum wa kuhakikisha usalama wao wakati wa safari hiyo. “Tumepanua wigo wa huduma zetu, hatufanyi tu uokoaji bali pia tunatoa huduma kwa watalii wanaofanya utalii wa anga,” aliongeza.
Hata hivyo, Dk. Daniel alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni dhana potofu kwamba huduma yao ni ya uokoaji tu. Amesema wanajitahidi kutoa elimu kwa umma ili kuelewesha kuwa huduma zao ni pana zaidi, zikihusisha pia utalii wa anga.
“Kuna changamoto ya kufikia watu wote, hasa watalii wenye bima za afya. Lakini tunajitahidi kuwasaidia watanzania wanaopanda milima na kufanya kazi za kubeba mizigo wanapopatwa na changamoto za kiafya, bila kujali gharama,” alisema.
Aidha, aliendelea kueleza kuwa mbali na uokoaji, Kili MediAir sasa imeongeza huduma za utalii wa anga, akitoa wito kwa watalii kufika kwa wingi nchini kujionea vivutio vya kipekee vilivyopo.
Kili MediAir kwa sasa inajikita zaidi katika Kanda ya Kaskazini, lakini ina malengo ya kufikia vivutio vyote nchini kwa lengo la kuboresha usalama na huduma kwa watalii.