Moshi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limezindua kampeni mpya yenye lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, kwa jina “Tuwambie Kabla Hawajaharibiwa.” Kampeni hii inalenga kuelimisha jamii kuhusu namna ya kuzuia ukatili huu kabla ya kuathiri watoto, huku vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vikiongezeka mkoani humo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi Asia Matauka, alieleza kuwa, licha ya kupungua kwa matukio ya ubakaji na ulawiti kutoka kesi 415 mwaka 2022 hadi 285 mwaka 2023 kwa kipindi cha Januari hadi Agosti, bado kuna haja ya kuongeza juhudi za elimu kwa umma ili kuzuia kabisa ukatili huu.
“Ingawa tumepokea kesi chache zaidi mwaka huu, hali bado si salama. Tunahitaji kuendelea kutoa elimu ili kuhakikisha vitendo hivi havitokei kabisa,” alisema Matauka. Pia, alibainisha kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinasababishwa na imani potofu za kishirikina, ambazo wazazi au walezi huamini kuwa vitendo hivyo vinaweza kuleta mafanikio.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, aliipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo muhimu na kueleza kuwa polisi wa sasa wamebadilika kutoka kuwa vyombo vya kutisha hadi kuwa watoa huduma kwa jamii.
“Polisi wa zamani walikuwa wanaogopwa, lakini sasa wamekuwa kimbilio la raia. Polisi wa sasa hawakamatishi wahalifu pekee, bali wanajukumu la kutoa ushauri na kuleta maendeleo ya kijamii,” alisema Mwangwala.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Malezi na Ulinzi wa Jamii Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro (SMAUJATA), Immaculata Mwigani, aliahidi ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kampeni hiyo, licha ya changamoto za ukosefu wa rasilimali.
“Hata bila magari na pesa, tunajitahidi kutembelea nyumba kwa nyumba kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia. Tatizo kubwa ni wazazi kuacha watoto bila uangalizi, jambo linaloongeza hatari ya watoto kukumbwa na ukatili,” alisema Mwigani.
Kampeni hii inalenga kufikia vijana wa shule za sekondari na vyuo vikuu ili kuwasaidia kujitambua na kujiepusha na vitendo vya ukatili. Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea kutoa elimu katika maeneo yote ya mkoa huo ili kulinda watoto na kuzuia ukatili kabla ya kuharibu maisha yao.
“Kampeni hii ni muhimu kwa kuzuia ukatili na kulinda maisha ya watoto wetu,” alihitimisha Mrakibu Matauka.