Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma akizungumza jambo wakatika akifungua Kongamano la Nne la Wanawake katika Uongozi lenye lengo la kujadili mada mbalimbali za kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala ya uongozi lililofanyika leo Oktoba 21, 2024 jijini Dar es Salaaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute Kadari Singo akizungumza jambo wakatika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Wanawake katika Uongozi lenye lengo la kujadili mada mbalimbali za kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala ya uongozi lililofanyika leo Oktoba 21, 2024 jijini Dar es Salaaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma amefungua Kongamano la nne la Wanawake katika Uongozi lenye lengo la kujadili mada mbalimbali za kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala ya uongozi, huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwa Rasilimali watu kama nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya Kitaifa na kukuza uchumi pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya Uongozi Institute ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mafunzo ya awamu ya tano na sita kwa viongozi wanawake, ambapo kwa mwaka huu lina dhima ya “Umuhimu wa Uongozi wa Mabadiliko kwa Viongozi Wanawake Barani Afrika”.
Akizungumza leo Oktoba 21, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la nne la Wanawake katika Uongozi, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika michakato wa uandaaji na utekelezaji wa mipango ya rasilimaliwatu, ajira pamoja na mafunzo.
Bi. Juma amesema kuwa Serikali imekuwa ikizingatia usawa katika upandishwaji na ubadilishwaji vyeo kwa kada mbalimbali pamoja na urithishanaji wa madaraka, uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kupunguza tofauti za uwakilishi kati ya wanawake na wanaume katika maamuzi.
“Ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuhakikisha usawa kati ya wanaume na wanawake, na takwimu zinaonyesha wanawake katika nafasi za uongozi wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na wakurugenzi katika taasisi mbalimbali za umma ni asilimia 28.6 ya viongozi wote” amesema Bi. Juma.
Ameeleza kuwa takwimu hizo zinaonesha ni kiashiria chanya kuelekea kufikia asilimia 30 ya uwakilishi wa wanawake katika uongozi, ambayo ni hatua muhimu kuelekea kufikia lengo Na. 5 la Usawa wa Kijinsia (SDG 5) kufikia asilimia 50 ifikapo 2030.
Bi. Juma amesema kuwa Serikali inatekeleza sera, mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 pamoja na mkakati wake wa 2005, mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa (2021/22-2025/26), na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
“Pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050, Mpango wa Tatu wa Maendeleo na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III), Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 pamoja na sera na mikakati mbalimbali ili kuimarisha usawa wa kijinsia na kuleta maendeleo jumuishi kwa wananchi” amesema Bi. Juma.
Ametoa pongezi kwa Taasisi ya Uongozi Institute kuwa kuandaa kongamano ambalo linatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha uongozi wa mabadiliko miongoni mwa viongozi wanawake.
“Naishukuru Taasisi ya UONGOZI kwa kunialika katika kongamano hili muhimu, niwapongeze kwa kuandaa na kutekeleza programu hii muhimu ya mafunzo kwa viongozi wanawake, pia nawapongeza viongozi wote wanawake kwa kuchaguliwa kujiunga na awamu ya tano na sita ya programu hii” amesema Bi. Juma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute Kadari Singo, amesema kuwa kongamano hilo limekutanisha wanawake viongozi kutoka nchi mbalimbali za barani Afrika wakiwa na lengo ni kujadili pamoja kuhusu wanawake na uongozi.
Singo amesema kuwa kongamano hilo linafanyika kila mwaka, huku akieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya uongozi umeonesha wanawake wengi wapo katika nafasi za chini za utendaji.
“Tumeanzisha program hii ili wanawake wawe na sifa za juu ambazo zitawafanya kuingia katika nafasi za maamuzi, tumeanza kutoa mafunzo tangu mwaka 2022 na kufanikiwa kuhitimu wanawake 199 mpaka sasa” amesema Singo.
Amesema kuwa sasa wanaingia darasa la tano na sita, huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa kushiriki kwani zaidi ya wanawake 1,500 waliomba kushiriki lakini nafasi zilizopo 100.
Singo amefafanua kuwa mafunzo hayo yanatolewa bure kwa washiriki, hivyo wanaendelea kutafuta wafadhili ili kuongeza idadi ya washiriki kila mwaka.