Wanafunzi wakiwa darasani wakipata mafunzo ya masuala ya fedha katika wiki ya huduma za kifedha inayoedelea kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe jijini Mbeya
Bw. Alphonce Bishanga kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Fedha Ndogo BoT akiwapa maelezo waalimu kutoka katika Saccos Yao jijini Mbeya waliofika katika banda Hilo kupata elimu.
………………
NA JOHN BUKUKU, MBEYA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewajengea uwezo wanafunzi wa shule mbalimbali mkoani Mbeya kwa kuwapatia elimu ya fedha, ikiwemo umuhimu wa kuweka akiba, uwekezaji wa hati fungani, na namna ya kuomba mikopo katika taasisi za fedha ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Akizungumza leo, Oktoba 22, 2024, na mwandishi wetu katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe jijini Mbeya, ambayo yana kauli mbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi,” Mchambuzi wa Masoko ya Fedha kutoka BoT, Bw. Francis Samweli, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya fedha.
Bw. Samweli amesema BoT inataka kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa mpana kuhusu masuala ya fedha na majukumu ya Benki Kuu, ikiwemo kusimamia mabenki yote nchini. “Wamekuja wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, wakiwemo kutoka Chuo cha TIA, na wamepata elimu ya uwekezaji kwenye hati fungani, ambazo ni dhamana za serikali. Wanafunzi wameonyesha mwamko mkubwa wa kutaka kujua zaidi kuhusu hati fungani na dhamana za muda mfupi jinsi zinavyofanya kazi,” alieleza Bw. Samweli.
Pia, aliongeza kuwa wanafunzi hao wamenufaika na elimu kuhusu mikopo, faida zake, pamoja na jinsi BoT inavyosimamia masuala ya uchumi, hususani dhamana za serikali ambazo zinatolewa wakati mwingine kwa wananchi.
Kwa upande wake, Bw. Alphonce Bishanga kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Fedha Ndogo katika BoT, amesema kuna faida kubwa ya kuwafundisha wanafunzi kwani wanakuwa mabalozi wa elimu ya fedha katika jamii. “Ni muhimu kwa wanafunzi kuanza kujifunza kuweka akiba wakiwa wadogo ili wakiwa wakubwa waweze kusimamia vizuri matumizi yao ya fedha,” alisema Bw. Bishanga.
Aliongeza kuwa wamewafundisha wanafunzi kuangalia taasisi za fedha wanazotaka kuomba mikopo, kuhakikisha taasisi hizo zipo chini ya usimamizi wa BoT, kuona leseni zake, na kupata mikataba rasmi.
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali mkoani Mbeya walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa wataalamu wa masuala ya fedha.