Na Seif Mangwangi, Arusha
WASHIRIKI wa kongamano la nne la kimataifa kuhusu changamoto ya umiliki wa Ardhi kwa vijana barani Afrika (CIGOFA4), wamesema migogoro ya kisiasa katika nchi nyingi barani humo imekuwa ikisababishwa na kukosekana kwa sera zinazotambua vijana katika umiliki wa rasilimali Ardhi.
Wakizungumza katika kongamano hilo washiriki hao zaidi ya 500 kutoka katika nchi 18 barani Afrika linaloendeshwa pia kwa njia ya Mtandao, wamesema ili migogoro hiyo iweze kumalizika ni wakati sasa kwa wakuu wa nchi Barani humo kutengeneza sera ambazo zitatoa majibu ya namna vijana watamilikishwa ardhi kwaajili ya kujipatia kipato.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Vijana kwa ajili ya Ardhi barani Afrika (YIALA) na Mwanzilishi wa Kongamano hilo, Innocent Antoine Houedji amesema bila utashi wa kisiasa kufanyika katika nchi za Afrika migogoro ya ardhi na vita vitaendelea kuwepo.
”Vijana ndio kundi pekee ambalo linaweza kubadilisha uelekezo wa kisiasa katika nchi zetu kwa kuwa wao ndio kundi kubwa miongoni mwa makundi mengine, hivyo tunahitaji mjadala wa kisiasa kuhusu namna vijana wataweza kumilikishwa Ardhi ili waweze kuitumia kuzalisha na kuingizia nchi zao uchumi.
“Kwa kufanya hivyo vijana watakuwa na ajira ya kudumu kupitia ardhi hiyo aliyomilikishwa na sasa ni wazi migogoro ya kisiasa itamalizika kwa kuwa hakutakuwa na kijana anayelalamika kwamba hana ajira kwa kuwa watakua bize kufanya uzalishaji, amani na usalama wa raia vitakuwepo,”amesema.
Houedji amesema kupitia mkutano huo, wajumbe watajadili ajenda hiyo ya utashi wa kisiasa kuhusu namna vijana watamilikishwa Ardhi, ambapo mbali ya kuhusisha vijana, pia watakuwepo watunga sera kutoka katika nchi mbalimbali barani Afrika na mwisho watakuja na mpango mkakati wa kuweza kutatua tatizo hilo.
Yidamno Wesley mwakilishi wa vijana kutoka shirika la Landesa nchini Liberia anasema kupitia shirika hilo wameweza kuanzisha programu inayokutanisha vijana na wazee kujadili namna ambavyo vijana wanaweza kumilikishwa ardhi na kuitumia kwaajili ya uzalishaji.
Amesema programu hiyo imefanikiwa kwa sehemu kubwa ambapo vijana wengi ambao walikuwa hawana uelewa wa thamani yao katika kupata haki ya kumiliki Ardhi wameitambua lakini pia Serikali na wazee katika jamii nchini humo na wenyewe wameanza kuelewa faida ya kumilikisha ardhi vijana.
Suzana Tuke kutoka shirika la Kinnapa wilayani Kiteto anasema ni haki ya vijana wa kike na wa kiume kumilikishwa Ardhi kwa kuwa ndio njia pekee ambayo itaweza kuondoa tatizo la ajira kwa vijana na kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Anasema ili kufanikisha hilo Serikali inatakiwa kutunga sera itakayoelezea namna ambavyo vijana watamilikishwa ardhi ambapo kupitia mkutano huo watajaribu kushawishi watunga Sera kukubaliana na hoja hiyo na kuweka mikakati ya namna ya kuifanikisha.
Kwa upande wake Theresia Raphael anayeshiriki mafunzo ya uongozi kupitia shirika la Kimataifa la International Land Coalition (ILC), anasema vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa elimu kuhusu umiliki wa Ardhi hivyo wakipewa elimu hiyo wataweza kufanya maendeleo makubwa.
Mkurugenzi wa shirika la Jumuiko la Maliasili nchini (TNRF) , Faustine Zakaria amesema vijana wengi wamekuwa wakikimbilia mijini wakiamini huko ndio kuna fursa za ajira kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu sahihi ya kuwawezesha kutumia ardhi kujipatia kipato.
Ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuangalia namna bora ya kuboresha mpango wake wa kilimo wa Bring Better for Tomorrow (BBT), kupitia wizara ya Kilimo kuwezesha vijana wengi kumilikisha ardhi na kuitumia kuzalisha huku ikitoa elimu kuhusu faida za umiliki wa Ardhi.
“Vijana wengi wamekuwa sio waaminifu, jamii inaamini ukimpatia kijana ardhi anaiuza lakini hii inasabishwa na mambo mengi sana ikiwemo vijana kutopewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya ardhi, kutokuwepo kwa miundo mbinu ya kumwezesha kutumia ardhi hiyo kuzalishia hivyo kinachotakiwa hapa ni elimu kwanza ndipo mambo mengine yaendelee,”amesema Faustine.