Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani Taifa (NECTA), Dkt. Said Mohamed, akizungumza a waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 22, 2024 wakati akitoa taarifa ya mitihani hiyo na kidato cha pili unaotarajiwa kuanza Oktoba 28,2024.
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza kuanza kwa mitihani ya Upimaji kwa darasa la nne na kidato cha pili kwa mwaka 2024 kwa siku tofauti na kuonya kuwachukulia hatua kali za kisheria watakao bainika kufanya udanganyifu
Watahiniwa 1,633,900 wanatarajia kufanya mitihani ya kujipima kitaifa ya darasa la nne (SFNA) inayoanza kesho Oktoba 23 katika shule za msingi 20,069 Tanzania Bara na kumalizika Oktoba 24,2024
Mitihani hiyo itafanyika kesho na kesho kutwa ikihusisha wavulana 794,021 sawa na asilimia 48.60 na wasichana 839,879 sawa na asilimia 51.40.
Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani Taifa (NECTA), Dkt. Said Mohamed, amesema hayo leo Oktoba 22, 2024 jijini Dar es Salaa. wakati akitoa taarifa ya mitihani hiyo na kidato cha pili unaotarajiwa kuanza Oktoba 28,2024.
Amesema ma baraza hilo halitasita kufuta matokeo ya mwanafunzi ambaye atajihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa mujibu wa kanuni za mitihani.
Ameelezea kuwa, wanafunzi 1,532,421 wa darasa la nne sawa na asilimia 93.79 watafanya upimaji kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 101,479 sawa na asilimia 6.21 watafanya upimaji kwa lugha ya kingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia.
“Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wapo 5,938, kati yao 1,185 wenye uoni hafifu, 132 wasioona, 1178 wenye ulemavu wa kusikia, 1800 wenye mtindio wa akili na 1643 wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” amesema.
Akizungumzia mitihani ya kidato cha pili, inayotarajiwa kuanza Oktoba 28,1014 na kumalizika Novemba 7,2024, Dkt. Mohamed amesema wanafunzi 869,673 wamesajiliwa kufanya upimaji huo mwaka huu.
Kati ya wanafunzi hao, wavulana 399,383 sawa na asilimia 45.92 na wasichana 470,290 sawa na asilimia 54.08.
Aidha wapo waanafunzi wenye mahitaji maalumu 1863 kati yao, 1053 ni wenye uoni hafifu, 83 wasioona, 540 wenye ulemavu wa kusikia, 137 wenye ulemavu wa viungo vya mwili na 50 wenye ulemavu wa akili.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa wanafunzi wa kujitegemea 9618 waliosajiliwa wavulana ni 3712 sawa na asilimia 38.59 na wasichana ni 5906 sawa na asilimia 61.41. Huku pia wanafunzi 66 wenye mahitaji maalumu kati yao wenye uoni hafifu ni 65 na asiyeona mmoja.
Amefafanua kuwa, hadi sasa maandalizi ya mitihani ya upimaji kwa watahiniwa wote yamekamilika ikiwemo kusambazwa karatasi za upimaji, nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo katika Halmashauru/Manispaa zote nchini.
Ametoa wito kwa wasimamizi walioteuliwa kusimamia upimaji huo, kufanya kazi yao kwa umakini, uadilifu wa hali ya juu.
“Wasimamizi wahakikishe wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi, kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake,” amesema.
Ameeleza kuwa, wasimamizi wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wanafanya upimaji kwa muda uliopangwa katika hali ya utulivu.
Amesema wamiliki wa shule hawatakiwii kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha upimaji huo na baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa Upimaji Kitaifa
Baraza hilo halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote ambaye atahusika kusababisha udanganyifu kwa mujibu wa sheria za nchi.